Ukikutwa na mfuko wa plastiki faini, kifungo

Ukikutwa na mfuko wa plastiki faini, kifungo

Muktasari:

  • Wasambazaji, watumiaji, wazalishaji na waingizaji wa vifungashio visivyokidhi vigezo kuanzia leo watakumbana na faini au vifungo vya vipindi tofauti, Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeeleza.

Dar es Salaam. Wasambazaji, watumiaji, wazalishaji na waingizaji wa vifungashio visivyokidhi vigezo kuanzia leo watakumbana na faini au vifungo vya vipindi tofauti, Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeeleza.

Hiyo ni baada ya matumizi ya vifungashio hivyo vya plastiki kufikia ukomo wake jana, miezi mitatu tangu aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ummy Mwalimu kutangaza kuwa jana ilikuwa mwisho wa matumizi ya vifungashio hivyo.

Vifungashio vinavyopaswa kutumika ni vile vyenye anuani ya mzalishaji, huku sifa nyingine ikitajwa kuwa na uwezo wa kufanyiwa urejelezwaji.

Jana katika mkutano uliowakutanisha wadau wa sekta hiyo, likiwamo Shirikisho la wenye viwanda Tanzania (CTI), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Nemc, ilielezwa kuwa, hadi sasa viwanda 30 vimeshapewa leseni ya kuzalisha vifungashio hivyo.

Mkurugenzi wa Nemc, Dk Samweli Gwamaka alisema watu watakaokutwa wakitumia vifungashio ambavyo havikidhi vigezo hivyo faini yake ni kuanzia Sh30,000 hadi Sh500,000.

“Kwa msambazi faini yake ni hadi Sh10 milioni au kifungo cha miaka mitatu hadi saba, huku wazalishaji na waingizaji faini yao ikiwa ni Sh5 milioni hadi Sh10 bilioni.

“Athari za vifungashio hivi ni zilezile za mifuko ya plastiki, hivyo tukaamua lazima tuweke viwango vitakavyotusaidia kupunguza kiasi cha mifuko kinachoenda katika ardhi na majini,” alisema.

Kemilembe Mntasa ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Idara ya Mazingira, alisema ili kuhakikisha mazingira hayaathiriwi na vifungashio hivyo, wako katika mchakato wa kuandaa viwango vya uzalishaji vifungashio vya plastiki vinavyooza.