Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Umejiandaa vipi na Januari?

Mungu amekupa neema ya kusogea mpaka mwishoni mwa mwaka 2024.

Neema ya Mungu hii inaweza pia kukusaidia ukaingia mwaka mpya.

Ili kuingia mwaka mpya, kwa mwajiriwa umebakisha mshahara wa mwezi wa 12 na kama ni mfanyabiashara umebakiza faida ya mwezi wa 12.

Mshahara na faida hizo za mwezi wa 12 vina kazi nyingi.

Kwanza kuna gharama na matumizi ya kawaida ya mwezi kama chakula, matibabu na usafiri. Pili kuna sherehe za mwisho wa mwaka.

Sherehe ambazo hutumia kiasi kikubwa cha kipato hicho na wakati mwingine huwa hakitoshi.

Baada ya sherehe za mwisho wa mwaka, kuna zile gharama za lazima za mwezi wa kwanza, mathalani gharama kama ada za watoto na kodi za nyumba.

Hizi ndizo hufika ambapo mtu anakuwa hana kitu kabisa kwa kuwa gharama za mwezi wa 12 zimemwacha hana kitu mfukoni na wakati mwingine akiwa na madeni makubwa.

Kabla ya kuanza kufikiria kodi na ada, mtu anafikiria kwanza jinsi ya kulipa madeni yatokanayo na sherehe za mwisho wa mwaka.

Akiwa anapambana na madeni hayo, muda wa shule kufungua unawadia.

Anafikiria jinsi ya kutatua hili la ada na kabla hajapata majibu yake, simu ya mwenye nyumba inaita.

Muda wa kodi nao umefika. Mtu anaishia kuchanganyikiwa. Haoni kipi afanye.

Ikitokea amepata pesa kidogo, anashindwa kuamua kipi atatue kwanza kati ya kulipa madeni, kulipa ada ama kulipa kodi ya nyumba.

Hii ni ngumu sana, hasa kwa wale wanaotegemewa katika familia.

Suala hili halina shida kabisa kwa wale wanaotegemea.

Wategemezi hawa mara nyingi huwa ndio sababu ya changamoto hii. Wategemezi huandika mahitaji yao ya sikukuu bila kujali uwezo wa baba yao.

Wanaandika bila kujua mshahara au kipato hicho cha mwezi wa 12 ndicho kitakachotumika mpaka kwenye maandalizi ya shule zao.

Hawaoni mwingiliano wa sikukuu na ada ya shule. Wao wanataka sikukuu.

Kama baba ama mtu unayetegemewa, unatakiwa kujiandaa kwa hili.

Kwa kuwa suala hili lilikutokea mwaka jana, hutakiwi kuruhusu likutokee kwa sasa, kwani kila mwaka mwezi wa kwanza unakuja, hutakiwi kuwa na mwezi wa kwanza wenye shida katika maisha yako yote. Mwaka huu unatakiwa kubadilika.

Unaweza kuamua kuondoa kabisa sherehe na kuwa siku ya kawaida kwa familia yako. Pesa hiyo itumike kwenye ada au kodi ifikapo mwezi wa kwanza.

Unaweza pia kupunguza sana matumizi ya kipindi cha sherehe ili kubakiza pesa.

Kitu kingine unachoweza kufanya ni kuwa na utaratibu wa kuweka akiba kidogokidogo kila mwezi kwa ajili ya matukio haya muhimu ya mwezi wa 12.

Kama unataka kufanya sherehe kubwa, unatakiwa kuanza kuandaa sherehe hiyo mwezi wa kwanza.

Unatakiwa kuwa unaweka kiasi fulani cha pesa kila mwisho wa mwezi.

Ifikapo mwezi wa 12 utafanya sherehe bila kuathiri mahitaji ya ada na kodi ifikapo mwezi wa kwanza.