Upungufu wa dagaa maumivu mapya Dar

Dar es Salaam. Huenda ukawa umeshtushwa na upungufu wa dagaa unaojitokeza kwenye baadhi ya masoko jijini hapa.

Hali hiyo imechagizwa na mwenendo wa mvua kubwa zinazoendelea nchini, kuathiri kiwango cha uzalishaji samaki katika Soko la Kimataifa la Samaki Ferry.

Mwananchi jana iliweka kambi katika soko hilo na kubaini ndoo moja ya lita 20 ya dagaa mchele imepanda kutoka wastani wa Sh40,000 hadi Sh70,000 ndani ya wiki mbili zilizopita.

Ndoo ya dagaa wakubwa imepanda pia kutoka wastani wa Sh25,000 hadi wastani wa Sh50,000.

Kutokana na mazingira hayo, wafanyabiashara wa dagaa wa kukaanga katika magenge jijini hapa wamesema bei ya fungu la Sh1,000 haitabadilika, isipokuwa wamelazimika kupunguza wingi wake.

“Wiki iliyopita nimenunua ndoo moja kwa Sh35,000, lakini leo nauziwa Sh80,000. Kwa hiyo fungu la dagaa litapungua zaidi ili kufidia gharama, kwani kuwapandshia wateja ghafla hawatakuelewa,” alisema Justa Anthony, mwenye genge eneo la Tabata Shule aliyefika sokoni hapo kwa ajili ya manunuzi ya ndoo mbili.

Asha Salumu, mwenye genge la kuuza dagaa maeneo ya Manzese alisema bei ya dagaa kwa mteja wake haitakiwi kubadilika kulingana na utamaduni uliozoeleka. “Ukibadili bei kutoka Sh1,000 hadi Sh2,000 lazima utapoteza wateja wengi sana, kwa sababu idadi kubwa ya watu ni wale wa maisha ya kawaida.

“Kwa hiyo tunalazimika kuchezea vipimo, kwa sasa kipimo kimepungua karibu nusu ya bei za awali, mteja atalalamika lakini hawezi kuacha kuja kununua kwa sababu ya kipato chake,” alisema.

Ushahidi wa mazingira hayo pia ulielezwa na Fabian Kakezi, anayesafisha samaki kwa miaka 25 sasa sokoni hapo, aliyesema samaki wamepungua sana kipindi hiki.

Hata hivyo, Mkuu wa Kituo cha Uvuvi katika soko hilo lenye wavuvi takribani 1,700, Ramadhani Mtabika alisema pamoja na bei hizo, uzalishaji wa samaki haujabadilika.

Uzalishaji wa Oktoba, 2023 mwaka huu ulikuwa tani 26 kwa siku, sawa na makadirio ya mwezi huu.


Mwenendo ulivyo

Mwenendo wa uzalishaji wa samaki huathiriwa na vipindi viwili. Kuna kipindi cha pepo za Kusi (kusini) kinachokuwa na upatikanaji wa samaki wachache kutokana na hali ya baridi pamoja na kipindi cha Kaskazi (Kaskazini) kinachokuwa na upatikanaji wa samaki wengi kutokana na uwepo wa joto la bahari.

Akilizungumzia hilo, Ofisa Uvuvi wa soko hilo, Abeid Shamte alisema mabadiliko ya hali ya hewa yanayokuja na mvua kubwa husababisha pia kupunguza uzalishaji wa samaki kama ilivyo mvua za kipindi hiki.

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imewatahadharisha wananchi kuwepo mwendelezo wa mvua kubwa mfululizo mwezi huu.