Wabunge wataka biashara za wazawa zilindwe
Muktasari:
- Imeelezwa kuwa, ulinzi wa biashara za wazawa ni jambo la msingi kwa kuwa baadhi ya viwanda vya wageni vimekuwa vikikutwa na upungufu wa kutengeneza bidhaa ambazo hazifikii viwango na ubora
Dodoma. Wizara ya Viwanda na Biashara imetaja vipaumbele saba ikiomba bajeti ya Sh137.8 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27 huku wabunge wakisisitiza ulinzi wa bidhaa za wazawa.
Waziri wa ya Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amewasilisha bajeti hiyo leo Ijumaa Mei 22, 2026 na kuvitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya viwanda, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma kwa kuboresha mazingira.
Vipaumbele vingine ni kuchochea maendeleo ya viwanda na biashara kupitia ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa, elimu na mafunzo ya ujuzi, kuimarisha upatikanaji wa fedha na mitaji kwa wajasiriamali na wazalishaji viwandani pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na kuchochea ukuaji wa sekta binafsi.
Akizungumza baada ya uwasilishwaji wa bajeti, mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby amesema ulinzi wa biashara za wazawa ni jambo la msingi kwa kuwa baadhi ya viwanda vya wageni vimekuwa vikikutwa na upungufu wa kutengeneza bidhaa ambazo hazifikii viwango na ubora.
Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabibyo, akizungumza wakati wa kuchangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis.
Shabiby amesema hiyo ni moja ya sababu zinazochangia majengo wakati mwingine kubomoka lakini inashangaza wanaokamatwa ni wauzaji badala ya wenye viwanda.
“Nchi hii mbona inaliwa hivyo, mgeni anakuja na Dola tano na briefcase (mkoba) halafu anapewa mradi na kisha anakopa fedha zetu, tukichelewa kumlipa anatudai riba, watu wanafanya biashara zinazofanywa na wazawa, tusipoangalia tutabadirika hata rangi,” amesema Shabiby.
Mbunge wa Buchosa (CCM), Erick Shigongo ameomba kutungwa kwa sheria ya kuwalinda wazawa kwa kuwa, wengi wanafunga bidhaa zao kutokana na muingiliano wa biashara na wageni.
Awali akiwasilisha bajeti Waziri wa Viwanda na Biashara, amesema: “Naomba nikazie na kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu mpango wa wizara ninayoisimamia wa kuanzisha vituo vya ubunifu na ukuzaji wa biashara kwa vijana kama nyenzo muhimu ya kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.”
Kapinga amesema vituo hivyo ni muhimu kwa kuwa vitawawezesha vijana wenye mawazo bunifu ya biashara kupata mazingira rafiki ya kubuni, kukuza na kuendesha biashara zenye ushindani katika soko la ndani na la kimataifa.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma.
Kuhusu Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Kapinga amesema kwa mwaka 2026/27, watatayarisha viwango 520 vya kitaifa katika sekta mbalimbali huku wakitarajia kutoa leseni ya ubora kwa bidhaa 1,200 kutoka katika sekta tofauti zikiwamo bidhaa za wajasiriamali wadogo.
Kapinga amesema shirika litasajili majengo, maeneo ya uzalishaji, uuzaji na usambazaji wa bidhaa za chakula na vipodozi 50,000, kusajili bidhaa 2,600 za chakula na vipodozi, kukagua na kutoa vibali 142,000 kwa bidhaa zitokazo nje ya nchi.
Amesema kati ya vibali hivyo, 42,000 ni kwa bidhaa zitakazokaguliwa nje ya nchi na vibali 100,000 ni kwa bidhaa zitakazokaguliwa nchini.
Kwa upande wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), amesema wizara inatarajia kusajili kampuni 22,586, majina ya biashara 38,870, alama za biashara na huduma 4,186, maombi ya hataza 98 na kutoa hataza 46.
“Kwa upande wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), tumejipanga kuimarisha utendaji wa mfumo wa stakabadhi za ghala kwa kusimamia ubora wa bidhaa zinazoingia na kutoka ghalani pamoja na utendaji wa waendesha ghala, wakaguzi wa ghala na meneja dhamana,” amesema Waziri Kapinga.
Liganga na Mchuchuma
Waziri Kapinga amesema wizara imekamilisha majadiliano na mwekezaji wa Kampuni ya Shudao Investment Group Company Limited (SDIG) kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Chuma cha Liganga na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga akijadiliana jambo na Naibu Waziri wake, Dennis Londo mara baada ya kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma.
Amesema mwekezaji huyo mpya ni kampuni inayomilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ambayo imeinunua kampuni ya awali ya Sichuan Hongda Group Company Limited (SHG) kwa lengo la kutekeleza mradi unganishi kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).
Amesema kutekelezwa kwa mradi huo kutawezesha nchi kuokoa matumizi ya Dola 1.22 bilioni za Marekani (Sh3.2 trilioni) zinazotumika kununua bidhaa za chuma kutoka nje ya nchi ikiwa ni bidhaa ya pili kwa matumizi makubwa ya fedha za kigeni.
Maoni ya kamati
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imetoa maoni 12 kwa bajeti hiyo ikiwamo kuiongezea bajeti wizara ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kutekeleza azma ya kuleta mageuzi ya kiuchumi.
Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Mariamu Ditopile amesema kutopatikana kwa wakati kwa fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo, kunasababisha utekelezaji wa miradi kusuasua na mingine kutotekelezwa kabisa.