Wajasiriamali 400 Ilala wafundwa

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam hii leo wameendesha mafunzo ya biashara,  elimu ya fedha na mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali vijana, wanawake na walemavu waliopo katika Manispaa  hiyo.

Mafunzo hayo yalilenga kuwaandaa ili waweze kutumia vema mikopo na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali pamoja na manispaa hiyo.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo yaliyowakutanisha  pamoja wajasiriamali zaidi ya 400, Ofisa Maendeleo ya Vijana kutoka Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, Sapiencia Masaga  alisema  mafunzo hayo yatawasaidia kwa kiasi kikubwa wajasiriamali hao kutumia vyema mikopo wanayoipata kutoka serikalini na halmashuri za jiji hilo ili kujikwamua kiuchumi kulingana na malengo ya mikopo hiyo.

“Licha ya jitihada kubwa inayofanywa na halmashauri zetu kwa kutoa mikopo kwa vikundi mbalimbali vya vijana, wakina mama na walemavu bado tumekuwa hatupati matokeo mazuri sana kwasababu wengi wa walengwa wamekuwa wakishindwa kutumia vema mikopo husika na matokeo yake wanashindwa kufikia malengo na zaidi wanashindwa kufanya marejesho. Tunawashukuru NBC kwa kuwa mafunzo haya yanalenga kuondoa hiyo changamoto,’’ alisema.

Kwa upande wake Meneja Ukuzaji Biashara wa Benki ya NBC, Isdory  Sebastian alisema benki hiyo imeshirikiana na halmashauri ya Manispaa ya Ilala katika kutoa mafunzo hayo ili kujenga uelewa wa kutosha kuhusu usimamizi bora wa kifedha, umuhimu wa bima mbalimbali ikiwemo za afya na biashara pamoja na namna bora ya kutunza akiba zao waweze kuendesha shughuli zao kitaalamu ili waepukane na hasara zinazoweza kukwamisha ustawi wa biashara zao.

“Katika mafunzo hayo benki ya NBC tumejitahidi sana kuhakikisha walengwa wanajengewa uelewa wa kutosha ili sisi kama benki tusiishie tu kuwahifadhia fedha zao wanapokopeshwa na hizi halmashauri bali pia tuwasaidie kuhakikisha hiyo mikopo inakuwa na tija kwa pande zote yaani halmashauri na wajasiriamali.’’

“Tunawashukuru sana manispaa ya Ilala tungependa na Halmashauri nyingine pia waige mfano huu kwasababu mikopo hii inahitaji elimu sahihi kwa walengwa ili waweze kujikwamua kutoka kwenye umaskini na zaidi pia waweze kurejesha hizo fedha ili zitumike kuwakopesha wahitaji wengine,’’ alisema

Wakizungumza kwenye mafunzo hayo, wajasiriamali Iddy Kaziulaya na Bahati Angetile walisema mafunzo hayo yatawasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuwajengea uwezo wa kibiashara kwa kuwa wengi wao wamekuwa wakishindwa kuendeleza vema mikopo hiyo kulingana na malengo kusudiwa hali inayochangiwa na kukosekana kwa elimu ya kutosha katika uendeshaji wa shughuli zao.

“Changamoto kubwa nayoiona kwasisi wanufaika wa hii mikopo ni kwamba wengi wanakopa kabla hawajawa na hata wazo la biashara matokeo yake pale tu wanapopatiwa fedha zinaishia kwenye mipango kabla ya utekelezaji wa mradi. Tunashukuru kupitia mafunzo haya wengi tutasaidiwa kufahamu namna ya kujinasua kwenye changamoto hii,’’ alisema Kaziulaya