Wakulima wa korosho Mtwara wauza tani 16,000 mnadani

Muktasari:

Wakulima wa zao la korosho mkoani Mtwara wameuza korosho zaidi ya tani 16,000 kupitia vyama vya ushirika vya TANECU na MAMCU katika mnada wa tano uliofanyika wilayani Tandahimba na Mtwara.

Mtwara. Wakulima wa zao la korosho mkoani Mtwara wameuza korosho zaidi ya tani 16,000 kupitia vyama vya ushirika vya TANECU na MAMCU katika mnada wa tano uliofanyika wilayani Tandahimba na Mtwara.

Katika mnada huo korosho za chama kikuu cha Tanecu kiliuza tani 6,887 kwa bei ya juu Sh2,001 na bei ya chini ikiwa ni  Sh1,930.

Chama Kikuu cha Mamcu waliuza tani 9,200 kwa bei ya juu Sh2,005 na bei ya chini Sh1,862.

Akizungumza kwenye mnada wa tano wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba & Newala Cooperative Union (TANECU), Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Patric Sawala amesema kuwa wakulima wanapaswa kukausha korosho na kuzipeleka ghalani zikiwa na ubora unaotakiwa sokoni.

“Tunazalisha korosho nzuri jambo la muhimu ni kuzingatia ubora hata mnunuzi anaangalia ubora na ubora unaangaliwa kwa mambo mengi kuanzia kwenye utunzaji uzalishaji na kiwango cha unyevu kinachokubalika,” amesema.

“Wakulima wahakikishe wanakausha vizuri korosho wapime korosho kabla ya kupeleka ghala kuu, ukipeleka korosho nzuri na hazina uchafu, zitaendendelea kuwa na ubora stahiki,” amesisitiza.

“Tunataka korosho zilizotoka vyama vya msingi zifike salama. Vyama vya msingi mkipokea korosho hakikisheni mnapima unyevu ili kuhakikisha kuwa tunaweka korosho zilizokauka nzuri ghalani,” alisema Kanali Sawala.

Akiuza korosho hizo Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (Tanecu), Karimu Chipola  alisema kuwa kazi yake kubwa ni kuuliza kwa wakulima kama wako tayari kuuza korosho hizo ambapo wanunuzi wamezitaka kwa Bei ya juu Sh2,001 na chini Sh1,930.

“Tuwaombe wanunuzi waone ubora wa korosho zetu watambue namna tunavyotumia gharama kubwa kupata bidhaa hiyo kisha waongeze bei ili angalau kumridhisha mkulima,” alisema Chipola.

Naye Halima Tamatama mkulima  wa zao la korosho kutoka Wilaya ya Tandahimba alisema kuwa bei wameipokea kwakuwa ndio hali ya soko ilivyo ni vyema wakulima wengine wakapelekea korosho sokoni.

“Ili upate pesa lazima upeleke korosho sokoni hakuna namna ndio bei zilipozopo sokoni kama kungekuwa na namna nyingine tungefanya lakini hatuna budi kuuza ili kutendelee na mambo mengine,” amesema.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi & Mtwara Cooperative Union (MAMCU), Siraji Mtenguka  alisema kuwa mnada huo umefanyika Kijiji cha Rwelu  Kata ya  Muungano Manispaa ya Mtwara Mikindani ambapo wameuza tani 9,200 kwa bei ya juu Sh2,005 na bei ya chini shilingi 1,862.