Wakulima wa tumbaku waaswa kukata bima ya mazao

Mkuu wa mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian mwenye ushungi akiangalia shamba lililoharibiwa na mvua ya mawe katika Kijiji cha Kipanga, wilayani Sikonge. Picha na Robert Kakwesi

Muktasari:

  • Wakulima wa tumbaku nchini wamehimizwa kuwa na bima ya mazao ili kuepuka kupata hasara pindi wakipata majanga.

Tabora. Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian, amewahimiza wakulima wa tumbaku mkoani Tabora kuwa na bima ya zao hilo ili kuepuka hasara pindi wanapopata majanga ya ukame au mvua za mawe.

Dk Buriana amesema hayo leo Februari 13, 2023 katika Kijiji cha Kipanga wilayani Sikonge baada ya kushuhudia mashamba ya tumbaku yaliyoharibiwa na mvua ya mawe.

Amesema kama wangekuwa na bima ya zao hilo angalau wangekuwa na uhakika wa kupata fidia ya hasara waliyopata.

"Kuanzia msimu ujao, tuanze kuwa na bima ya mazao likiwemo la tumbaku ili yakitupata kama hili la mvua ya mawe, basi tusipate hasara zaidi," amesema.

Pia amewaahidi wakulima hao kuwa atapeleka taarifa zao ngazi za juu ili kuona kama kuna fungu au uwezekano wa kusaidiwa wa kupunguza makali ya hasara waliyopata.

Kiongozi huyo amewataka waatalamu wa kilimo kusaidia ili hasara isiwe kubwa hasa kwa zile ekari ambazo zao hilo halijaharibika sana.

Awali Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Ngulu, Gile Cheja, amemweleza Dk Burian kuwa wanachama wao wamepata hasara baada ya mvua ya mawe kuharibu ekari 72 ambazo kati ya hizo, ekari 15 zimeharibiwa kabisa.

Hata hivyo, amesema kufahamu hasara iliyopatikana na kwamba tathmini inaendelea kufanyika.

Naye Meneja mkuu wa Chama cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU), Samwel Jokea, amesema kwa sasa kuna vyama vya msingi 169 wanavyosimamia, akisema wanaangalia hasa iliyopatikana.