Wakulima watakiwa kuingia makubaliano mauzo ya korosho

Muktasari:

  • Serikali ya Mkoa wa Mtwara imesikitishwa na taarifa za korosho zaidi ya tani 245 za vyama vya ushirika vya Mamcu na Tanecu kutouzwa mnadani, hali iliyowaacha njiapanda wakulima.

Mtwara. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanal Ahmed Abbas ametaka kuwe na makubaliano kati ya vyama vya ushirina na wakulima kabla korosho hazijauzwa ili kuepuka hasara.

Agizo hilo limetolewa wakati kukiwa na taarifa za korosho zaidi ya tani 245 za vyama vya ushirika vya MAMCU na TANECU kutouzwa mnadani, hali iliyowaacha njiapanda wakulima.

Akizungumza leo Februari 13 katika kikao cha kujadili kilimo mkoani humo, Kanali Abbas ameleza kusikitishwa na hali hiyo na kutaka hatua za haraka zichukuliwe.

“Inaumiza mkulima anatumia nguvu nyingi kuandaa shamba anavuna kisha anakaa anasubiri soko la awali ambalo hana uhakika nalo wala hana makubaliano nalo hii sio sawa,” amesema Kanal Ahmed.

Awali akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mtwara Masasi Coperatvie Union (MAMCU), Biadia Matipa amesema mpaka anafika katika kikao hicho zaidi ya tani 200 zimebakia kwenye vyama vya msingi.

 “Ili kumnurusu mkulima ambaye korosho zake zimekaa bila kupata pesa tunaomba Bodi ya Korosho (CBT) ichukue hatua za haraka kupata wateja wa korosho kwa kuwa zikifika katika msimu ujao zitashuka ubora na zitauzwa kwa bei ya hasara,” alisema Matipa

Naye Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba & Newala Cooperative Union (Tanecu) Mohamed Mwinguku amesema kuwa soko la awali lina changamoto nyingi.

“Mtu anakwenda kununua soko la awali Sh1, 600 na sisi tumeuza Sh1, 800 kwenye minada wengi wanenda huko ili kukwepa baadhi ya tozo, kwa mfano hawalipii pembejeo, halipii magunia wala ushuru kama ulivyokwenye minada huo ni mgongano,” amesema.

Kwa upande wake Meneja wa Kiwanda cha Amama Farmers Limited, Mwakalinga Yassin amesema ununuzi wa korosho katika soko la awali hauna tatizo kama lipo wakae walitatue.

 “Nawaomba vyama vikuu kama kuna changamoto tukae tuzitatue wote tunaenda sehemu moja ili kuongeza ubanguaji nchini lazima tushirikiane na viwanda vidogo vidogo tusaidiane wote ni wa moja na tunataka kuendeleza mkoa wetu sio ugomvi,” amesema Mwakalinga

Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Alfred Francis alisema kuwa lengo nikutaka kuongeza ubanguajia nchini ndio maana tulianzisha soko la awali.

“Soko la awali ni hiari kwa mkulima kuuza sio lazima, wapo wakulima wamevuna kilo 50 ama chini ya hapo tunamruhusu kwa hiari yake kuziuza katika soko hilo kwa ngazi ya Amcos (Chama cha Msingi cha Ushirika) ili kusimamia uuzwaji wake na tozo na pia kuna makubaliano kati ya mnunuz na mkulima,” amesema.