Washindi Vodacom Digital Accelerator kutangazwa

Muktasari:

  • Kampuni ya Vodacom Tanzania PLC inatarajia kutangaza kampuni tatu bunifu chipukizi zitakazoibuka washindi wa msimu wa pili wa programu ya Vodacom Digital Accelerator inayofanyika kwa kushirikiana na Smart Lab.  

Dar es Salaam. Kampuni ya Vodacom Tanzania PLC inatarajia kutangaza kampuni tatu bunifu chipukizi zitakazoibuka washindi wa msimu wa pili wa programu ya Vodacom Digital Accelerator inayofanyika kwa kushirikiana na Smart Lab.  

Tukio hilo linatarajiwa kufanyika Machi 3, mwaka huu katika hoteli ya Hyatt Regency ya jijini hapa baada ya washiriki kuwasilisha na kuonyesha shughuli wanazozifanya kwa jopo la majaji kwenye maeneo ya teknolojia, ujasiriamali, uwekezaji, na sheria.

Msimu wa pili wa programu ya Vodacom Digital Accelerator ulianza mwezi Aprili mwaka jana na kuruhusu maombi kutoka kwa kampuni bunifu chipukizi za kiteknolojia za Kitanzania ambazo zinakua.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari leo Machi Moshi, imemnukuu Mkurugenzi wa Huduma za Kidigitali, Vodacom Tanzania, Nguvu Kamando, akisema baada ya mchujo kufuatia mamia ya maombi yaliyopokelewa, kampuni 12 zilichaguliwa kujiunga na programu wakijengewa uwezo wakipatiwa msaada wa kukuza mikakati yao kimasoko, kiufundi na kuwaunganisha kwa washirika na wawekezaji.     

Kampuni hizo bunifu chipukizi zinatoka kwenye sekta tofauti ambazo ni pamoja na huduma za kiteknolojia za kifedha, afya, biashara za mtandaoni, elimu, kilimo, na usalama wa mtandaoni.

“Tumefurahi kufikia hatua hii ya programu yetu ya Vodacom Digital Accelerator ambapo tumefanikiwa kuona namna ilivyosaidia kukuza ubunifu kwa kampuni chipukizi za Kitanzania,” amesema

Kamando amesema uwasilishaji utakaofanyika Machi 3, kwenye maonyesho hayo ndio utasaidia kuwapata washindi watatu, ambao watazawadiwa zaidi ya Sh200 millioni pamoja na uwezekano wa uwekezaji zaidi mbeleni.

“Ningependa kutoa wito kwa wadau kwenye sekta ya ubunifu na teknolojia kujisajili kwa njia ya mtandaoni ili kushiriki wakiwa popote walipo,” amesema Kamando.

Pia amesema watu wote wanakaribishwa kujiunga na kusikiliza uwasilishaji wa maonyesho hayo ili waweze kuzipigia kura kampuni bunifu chipukizi bora kupitia kiambatanisho (link) ambacho kitapatikana kwenye kurasa rasmi za mitandao ya kijamii ya kampuni.

Kampuni bunifu chipukizi ambazo zimefikia hatua ya fainali ni pamoja na Shule Yetu Innovations, Smart Darasa, Lango Academy na Vijana Tech, ambazo ni upande wa huduma za elimu za kiteknolojia, huku Hack it Consultancy ikiwakilisha eneo la huduma za usalama wa mtandaoni.

Nyingine ni Seto, Twenzao, Get Value, na Spidi Africa zipo chini ya biashara za mtandaoni wakati Medpack ikiwakilisha huduma za afya za kiteknolojia, huku Bizy Tech Pamoja na Bizzy Pay zipo upande wa huduma za kifedha za kiteknolojia.