Zanzibar kutumia mfumo wa kielektroniki kukusanya kodi

Monday April 05 2021
Kodi pc
By Alex Nelson Malanga

Dar es Salaam.  Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) imetangaza kuanza kutumia teknolojia ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato inayotwa `Virtual Fiscal Devices’ (VFD), ukiwa ni mkakati wa kukuza ukusanyaji wa mapato visiwani humo.

Kamishna wa ZRB, Salum Yusuf Ali alisema wiki iliyopita kuwa tekinolojia hiyo inayotarajia kuanzia mwezi huu itawezesha kupandisha ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 20 na itaviwezesha visiwa vya Zanzibar kuachana na njia za kawaida za ukusanyaji wa mapato.

Amesema kupitia VFD na stempu za kielektroniki (ETS) ambazo pia ziko mbioni kutumika visiwani humo na zitaongeza ukusanyaji wa mapato kufikia Sh55 bilioni kutoka Sh46 bilioni zinazokusanywa sasa.

“Mambo mengine yatabaki kama kawaida, tuna uhakika wa kufikia lengo kuanzia mwaka wa fedha wa 2021/22 kuanzia Julai,” amesema Ali kupitia mahojiano yaliyofanywa kwa simu.
Ametoa matumaini ya kuongezeka kwa mapato kutoka kwenye sekta ya utalii ambayo ndiyo inategemewa visiwani humo.

Jumla ya watalii 29,128 waliingia katika visiwa hivyo hadi Novemba 2020 ikilinganishwa na watalii 12,157 walioingia Oktoba kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu ya Zanzibar.
Hata hivyo, idadi ya watalii wa Novemba 2020 ni asilimia 61 ya watalii 47,824 waliotembelea Novemba 2019.

Lakini Ali anaona mwanga wa matumaini kutoka shimoni akitumaini kuwepo kwa maboresho katika sekta za kiuchumi.
Amesema mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa kodi itaziba mianya ya uvujaji wa mapato kwa sababu mifumo hiyo itakuwa ikipeleka taarifa moja kwa moja ZRB kwa hiyo itakuwa inajua miamala inavyofanyika.

Advertisement

Ni tofauti na risiti za karatasi zinazotumiwa ambazo ni rahisi kukwepa kodi.

Kampuni ya kimataifa ya Tehama kutoka Norway (NRD) na kampuni nyingine za ushauri zimeshinda tenda ya kufunga mfumo wa VFD na ETS visiwani humo.

Ali amesema wanafanya kazi na kampuni hiyo kuhakikisha udhaifu ulionekana katika majaribio yaliyofanyika kati ya Agosti na Desemba unadhibitiwa.

Majaribio hayo yalihusisha Kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa wafanyabiashara wapatao 300.

“Tulipanga kuzindua VFD mapema zaidi itakayosimamia zaidi ya VAT lakini hatukuweza kutokana na maambukizi ya Covid-19,” amesema Ali aliyetaja baadhi ya kopdi zitakazosimamiwa na mfumo huo kuwa pamoja na Ushuru wa Forodha, kodi ya kusafirisha nje na kodi za usafiri wa ndege.

“Kutokana na kuzuiwa kwa safari kulikowekwa na nchi mbalimbali ili kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo, timu ya mafundi kutoka Norway ilishindwa kufika mapema kufunga mfumo na kushughulikia udhaifu uliokuwepo,” aliongeza Ali.

Amesema kutokana sababu hiyo, wataalamu wa mfumo wa Stempu za kielektroniki (ETS) bado hawajafika, hivyo wanashindwa kusema wataanza lini.

“Siwezi kusema moja kwa moja ETS itaanza lini kwa sababu hata majaribio hayajaanza,” amesema Ali.

Uamuzi wa Zanzibar kutumia mfumo wa ETS unakuja wakati upande wa Bara ulishaanza kuutumia miaka miwili iliyopita.

Advertisement