Dunia yatikiswa mauaji ya jenerali wa Iran
Dunia imetikisika baada ya majeshi ya Marekani kufanya shambulio nchini Iraq na kumuua jenerali wa jeshi la Iran, Qasem Soleimani, baadhi wakihofia kuwa huo unaweza kuwa mwanzo wa vurugu Mashariki ya Kati, huku wabunge wa Marekani wakitofautiana.
Bei ya mafuta ilipanda ghafla na bei katika masoko ya hisa kuanguka baada ya mauaji hayo ambayo yamezua hali ya wasiwasi, huku Marekani ikiita nyumbani raia wake.
Marekani ilifanya shambulio hilo jana asubuhi wakati makombora yake yalipoelekezwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad na kumuua Soleimani pamoja na naibu wake, Abu Mahdi al-Muhandis.
Uamuzi wa Marekani kufanya shambulio hilo dhidi ya kikosi cha wanamgambo wa Hashed al-Shaabi, ambao ni sehemu ya jeshi la Iran, ulitokana na kundi la wananchi wa Iraq wanaoiunga mkono Iran kushambulia ubalozi wa Marekani kupinga mashambulizi yaliyofanywa na taifa hilo kubwa dhidi yake.
Muda mfupi baada ya mauaji hayo, kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei alimteua Esmail Qaani kuwa kamanda mpya wa kitengo cha nje cha jeshi hilo la kimapinduzi la Iran kutokana na kifo cha Soleimani.
“Kutokana na mauaji ya kiongozi wetu mtukufu, Jenerali Qasem Soleimani, namtangaza Brigedia Jenerali Esmail Qaani kuwa kamanda mpya wa Quds Force,” Ayatollah Ali Khamenei alisema katika taarifa yake.
Lakini dunia haijazipokea vizuri taarifa za mauaji hayo.
“Mauaji ya kamanda mkuu wa jeshi wa Iran yameifanya dunia kuwa hatari zaidi,” alisema waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Amelie de Montchalin ambaye anahusika na mambo yanayohusu bara la Ulaya.
Waziri huyo ametaka juhudi zifanyike kupunguza kukua kwa mgogoro Mashariki ya Kati.
“Tumeamka na kukuta dunia imekuwa hatari zaidi,” alisema alipoungumza na redio ya RTL, akisema Rais Emmanuel Macron atawasiliana wakati wowote na viongozi katika ukanda huo.
“Katika operesheni kama hii ni wakati tunapoweza kuona kukua kwa mgogoro kuko mbioni, tunachotaka zaidi ya yote ni amani na kuzuia kukua kwa mgogoro,” alisema Montchalin.
‘Inaanzisha vita ya kutisha’
Shambulio hilo pia limeishtua Iraq ambayo mauaji hayo yamefanyika kwenye ardhi yake, na kaimu waziri mkuu wa nchi hiyo, Adel Abdel Mahdi alisema kitendo hicho cha Marekani ambacho pia kimesababisha kifo cha kamanda wake, ni uvamizi ambao utaanzisha vita ya kutisha. “Mauaji ya kamanda wa jeshi katika nafasi yake rasmi ni uvamizi dhidi ya nchi ya Iraq, utaifa wake, serikali yake na watu wake,” alisema katika taarifa yake.
Abdel Mahdi alisema shambulio hilo ni ukiukwaji wa masharti ya kuwepo kwa majeshi ya Marekani katika ardhi ya Iraq.
Nchini Syria, serikali imeituhumu Marekani kwa kujaribu kuchochea vurugu katika Mashariki ya Kati.
Syria ina “uhakika kuwa kitakachotokea kutokana na uvamizi huu wa kijinga wa Marekani ni kuimarisha ujasiri wa kufuata njia za viongozi waliouawa kwa sababu ya imani yao,” waziri wa mambo ya nje alikaririwa na shirika la habari la Sana.
Nchini Marekani, shambulio hilo limeligawa Bunge; upande wa chama tawala cha Republican ukiunga mkono huku Democratic wakipinga.
“Katika kuonyesha kutatua tatizo na nguvu yetu, tulimpiga kiongozi wa wale wanaoshambulia maeneo huru ya Marekani,” alisema Kevin McCarthy, mbunge wa Republican.
Kauli yake ilifanana na ya wabunge wengine wa Republican. “Wow - zawadi ya kuua na kujeruhi Wamarekani imepanda kwa haraka,” alisema senata Lindsey Graham, mshirika wa karibu wa Trump, akiandika katika akaunti ya Twitter.
Shambulio dhidi ya Soleimani, ambalo lilitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad leo asubuhi nchini Iraq, pia lilimuua naibu kiongozi wa kundi la Hashed al-Shaabi, ambalo ni la wanamgambo.
Shambulio hilo limekuja baada ya watu wanaoiunga mkono Iran kuvamia ubalozi wa Marekani kupinga kitendo cha taifa hilo kubwa duniani kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya kikundi hicho.
Marekani ilifanya mashambulizi kujibu shambulio la makombora ya roketi yaliyofanywa siku chache kabla na ambayo yalimuua mkandarasi wa Marekani aliyekuwa akifanya kazi nchini Iraq.
Kwa kawaida Ikulu ya Marekani, inayojulikana zaidi kama White House, hutoa taarifa kwa wabunge waandamizi wa vyama vyote katika chombo cha Seneti na wawakilishi kabla ya shambulio lolote kubwa la kijeshi.
Lakini mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Eliot Engel alisema katika taarifa yake kuwa shambulio “lilifanyika bila ya taarifa au mashauriano na Bunge.”
Soleimani alikuwa “mbunifu mkuu wa vurugu kubwa” na ambaye “ana damu za Wamarekani mikononi mwake,” mbunge huyo wa Democratic alisema.
Lakini “kuendelea na kitendo cha ukubwa huu bila ya kulitaarifu Bunge ni tatizo kubwa kisheria na ni kudharau nguvu za Bunge kama sehemu ya serikali,” alisema Engel.
Hali kwa upande wa Democratic ilikuwa ya kupinga vikali shambulio hilo, huku spika wa Bunge, Nancy Pelosi akisema kumuua kiongozi wa juu wa kijeshi kunachokoza kuongezeka kwa vurugu.
“Marekani na dunia haiwezi kuvumilia hali hii ya wasiwasi kuendelea hadi kufikia sehemu isiyovumilika,” alisema katika taarifa yake.
Wagombea urais katika kampeni za mwaka 2020 pia walikuwa wakipima suasa hilo.
Joe Bidden, ambaye anaongoza kundi la wagombea urais kutoka Democratic, alisema Rais Trump amewasha moto.
“Hakuna shaka Iran italipiza kisasi. Tunaweza kuwa mwanzoni mwa mzozo mkubwa Mashariki ya Kati,” alisema Biden.
Katika hatua nyingine, Uingereza imetaka utulivu baada ya shambulio hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje, Dominic Raab alisema nchi hiyo “mara zote inatambua tishio linalotokana na Soleimani na kikosi chake cha Quds Force” na kuongeza kusema: “Kutokana na mauaji hayo, tunazishauri pande zote kutokuza suala hilo. Migogoro zaidi si kitu tunachopenda.”
Wakati hali ikizidi kuwa mbaya kisiasa, masoko ya hisa yalitikiswa na shambulio hilo kutokana na wawekezaji kuingiwa na hofu.
“Kwa kuangalia mwaka mpya ulivyoanza, masoko yalikuwa katika hali mbaya baada ya Marekani kumuua kiongozi mwenye ushawishi mkubwa wa Iran, Jenerali Qasem Soleimani,” alisema mchambuzi wa Spreadex, Connor Campbell.
Majeshi ya pamoja na Nato yalikuwa yakifuatilia hali nchini Iraq, yakitupia jicho mazoezi ya vikosi vyake. Nato imebakiza askari wachache nchini Iraq kwa ajili ya kufundisha majeshi ya serikali na umoja huo haukuhusishwa katika shambulizi lililomuua Soleimani.