Moto wa msituni wateketeza watu 112 Chile

Mabaki ya nyumba zilizoteketea kwa moto eneo la Vina del Mar, Chile Februari 4, 2024. Picha na AFP

Muktasari:

Mamlaka nchini Chile imesema takribani watu 112 wamekufa kutokana na moto uliozuka msituni

Chile. Takribani watu 112 wamekufa kutokana na moto uliozuka msituni katika eneo la Valparaíso nchini Chile.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la BBC, Rais wa Chile, Gabriel Boric ametangaza hali ya hatari akisema atatoa mahitaji yote muhimu kukabiliana na madhara yaliyosababishwa na moto huo uliozuka Ijumaa, Februari 2, 2024.

Inaelezwa tukio hilo ni baya zaidi kuwahi kutokea nchini humo.

Mamlaka imesema wengi wa walioathiriwa walikuwa mapumziko katika eneo la pwani wakati wa likizo ya majira ya joto.

Wizara ya Afya ya Chile imesema itaajiri wanafunzi wa udaktari wanaokaribia kumaliza masomo kusaidia kuondoa upungufu wa wataalamu.

Huduma za uokoaji zinakabiliwa na changamoto ya kuyafikia maeneo yaliyoathirika zaidi.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Carolina Tohá amesema huenda idadi ya vifo ikaongezeka.

Serikali imetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu safari kwenye maeneo yaliyokumbwa na moto huo.

Akizungumza na shirika la habari la AFP, Rodrigo Pulgar, aliyeshuhudia moto huo, amesema alijaribu kumsaidia jirani yake lakini akagundua nyumba yake imeanza kuungua.

"Jivu lilikuwa limetapakaa," amesema Pulgar.

Amesema wakazi wengi wa El Olivar ni wazee, na kwamba jirani yake alifariki dunia kwa sababu hawakuweza kumsaidia kutoka ndani.

Wizara ya Nyumba imesema kati ya nyumba 3,000 na 6,000 zimeathiriwa na moto huo.

Jumamosi, Februari 3, 2024 amri ya kutotoka nje iliwekwa kwa wale walio maeneo ya Viña del Mar, Limache, Quilpué na Villa Alemana.

Rais wa Chile, Boric amesema amri hiyo itasaidia kufungua njia na kuruhusu magari ya dharura kufika maeneo yaliyoathiriwa.


Waziri wa Mambo ya Ndani katika hotuba yake kwa Taifa, amesema askari wa Zimamoto 1,400 wamepelekwa eneo la maafa Jumapili Februari 4, 2024.

Pamoja nao wapo watu wa huduma za dharura, huku chanzo cha moto huo kikichunguzwa.

Moto huo umezuka kilomita 116 kutoka mji mkuu Santiago, katika mji wa pwani wa Valparaíso ambao hukusanya idadi kubwa ya watalii wakati wa kiangazi.

Mwaka jana, maeneo ya Biobío na Ñuble Kusini zaidi kutoka Valparaíso yalifikwa na maafa ya moto.

Imeandikwa kwa msaada wa mtandao.

Mwisho.