Papa Benedict XVI kuzikwa leo

Vatican. Kanisa Katoliki duniani lina taratibu zinazohusu vifo vya papa na mazishi yake, lakini zimeundwa mahsusi kwa ajili ya vifo vya mapapa walio madarakani.

Kwa kuzingatia ombi la aliyekuwa Baba Mtakatifu wa kanisa hilo, Benedict XVI la kuwapo kwa mazishi rahisi, serikali za Ujerumani na Italia pekee ndizo zitaalikwa kutuma wajumbe rasmi.

Ingawa wawakilishi kutoka nchi na mashirika mengine wanaweza kushiriki kwa nafasi binafsi.

Baba Mtakatifu Benedict ambaye ni mzaliwa wa Ujerumani, awali alijulikana kama Kardinali Joseph Ratzinger, aliishi Italia kwa zaidi ya miaka 40 kuanzia 1981.

Atazikwa leo katika basilica karibu na lilipo kaburi la Baba Mtakatifu Petro.

Pamoja na kwamba ni nchi mbili tu zitatuma wajumbe rasmi, nchi mbalimbali duniani zimeshatuma salamu za rambirambi.

Argentina

Balozi wa Argentina nchini Brazil, Daniel Scioli alimtaja Benedict kama mwanatheolojia mahiri, huku Gavana wa Cordoba wa nchini humo, Juan Schiaretti akisema Benedict XVI katika maisha yake alijitolea kwa ajili ya Kanisa.

Katika salamu zake za rambirambi, Rais wa Austria, Alexander Van der Bellen amesema atamkumbuka Benedict XVI kwa kuwaunganisha Waaustria kwa njia maalumu.

Askofu Mkuu wa Sydney, Anthony Fisher alisema Benedict XVI alikuwa mpole zaidi kuliko watu wote.

“Nililiona hili katika mikutano yangu kadhaa pamoja naye. Mwishowe, jambo la muhimu kwake lilikuwa ni kuwa mwaminifu kwa Yesu Kristo na kuwa na upendo kwa watu wa Kristo, na kwamba yeye alifanikiwa katika hilo.”

Canada

Waziri Mkuu, Justin Trudeau alisema Benedict XVI alikuwa mwanatheolojia na msomi aliyekamilika na alikuwa na msukumo na ushawishi kwa mamilioni ya watu duniani.

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani nchini Canada, Pierre Poilievre alisema Benedict XVI alitoa huduma ya unyenyekevu na utajiri wa kitheolojia kwa waamini Wakatoliki bilioni moja.

Wakati Poilievre akiyasema hayo, Askofu Raymond Poisson, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Canada, alisema Benedict XVI ameacha urithi mkubwa wa mafundisho ambayo yataendelea kuwatia moyo.

Uingereza

Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak alitoa taarifa, akisema alihuzunishwa na kifo cha Papa Emeritus Benedict XVI. “Alikuwa mwanatheolojia mkuu ambaye ziara yake ya Uingereza mwaka 2010 imeacha historia kwa Wakatoliki na wasio Wakatoliki nchini humo,” alisema.

Askofu Mkuu wa Canterbury, Justin Welby alisema kiongozi huyo alimtazama Yesu Kristo na kumfanya mzizi wa mawazo yake na msingi wa maombi yake kwa watu wote duniani.

Rais, Emmanuel Macron alisema baba mtakatifu huyo alifanya kazi kwa nafsi na akili kwa ajili ya ulimwengu wa kindugu zaidi.

Huku Rais, Frank-Walter Steinmeier katika taarifa yake, amesema Ujerumani inaomboleza kifo cha Papa Benedict XVI na itazikumbuka kazi zake.

Alisema ulimwengu umempoteza mtu aliyekuwa na imani kubwa ya kidini na mwanatheolojia mwenye hekima.

Kansela wa zamani, Angela Merkel amesema uamuzi wake wa kujiuzulu (mwaka 2013), alitoa ishara kwamba hata papa alilazimika kukabiliana na mzigo wa umri.

Rais Markus Soder wa Bavaria, ambaye ni mkuu wa jimbo alilozaliwa Benedict, alimesema wanamuomboleza Papa huyo wa Bavaria kwa sababu jamii imepoteza mwakilishi mwaminifu wa Kanisa Katoliki na mmoja wa wanatheolojia mashuhuri zaidi wa karne ya 20.

Georg Batzing, mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Ujerumani, alisema maaskofu wa Ujerumani wanaomboleza kumpoteza mtu ambaye alitoa tumaini na mwelekeo kwa Kanisa hata katika nyakati ngumu.

Ireland

Rais Michael Higgins alitoa taarifa akisema Papa Benedict XVI “atakumbukwa pia kwa thamani aliyoiweka kwa kazi ya kiakili na kwa kujitolea kwake binafsi katika Kanisa Katoliki la Roma, kazi hii iheshimiwe na wafuasi wote wawili, wakiwamo hata na wakosoaji.”

Israel

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alitoa tamko kwa niaba ya raia wote wa Israel akituma salamu za rambirambi ulimwengu kutokana na kifo cha Papa Benedict XVI, alisema Papa Benedict alikuwa kiongozi mkuu wa kiroho ambaye alijitolea kikamilifu kwa upatanisho wa kihistoria kati ya Kanisa Katoliki na Wayahudi, utamaduni aliouendeleza katika ziara yake ya kihistoria nchini Israel mwaka wa 2009.”

Italia

Rais Sergio Mattarella katika taarifa yake alisema Benedict XVI alikuwa mwanatheolojia mashuhuri, msomi mahiri na mtu wa utamaduni mzuri sana.

Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni alimtaja Benedict XVI kama “jitu la imani na akili” na kwamba ametoa maisha yake kwa huduma ya kanisa la ulimwengu na kuzungumza na mioyo ya watu na ataendelea kufanya hivyo.

Matteo Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu wa Italia, alisema maisha yake yalitegemea upendo kama onyesho la uhusiano wake na Mungu. Katika sehemu ya mwisho ya kuwapo kwake, aliufanya uhusiano huu na Bwana (Yesu) uonekane. Tunamshukuru Bwana (Yesu) kwa zawadi ya maisha yake na huduma yake kwa Kanisa.

Uholanzi

Waziri Mkuu Mark Rutte alisema, “kwa kifo cha Papa Benedict XVI, Kanisa Katoliki la Roma na Wakatoliki wote ulimwenguni kote wanapoteza kiongozi muhimu wa kiroho na kiakili. Tunamkumbuka kwa heshima.”

Palestina

Rais Mahmoud Abbas katika telegramu ya salamu za rambirambi alisema, “tunaomboleza kifo chake kwa pamoja, tukikumbuka mapokezi yetu ya utakatifu Wake huko Bethlehemu, mahali pa kuzaliwa Kristo, siku ambayo alikuwa mgeni mpendwa katika nchi takatifu Mei 2009, akibeba ujumbe wa upendo na amani kwa ulimwengu.

Katika ziara yake hiyo, alikutana na viongozi wa Kiislamu na Wakristo wa Palestina katika Hekalu Tukufu katika mji mkuu wetu Yerusalem na Kambi ya Aida kwa ajili ya wakimbizi wa Kipalestina, na alieleza mshikamano wake na kuunga mkono uhuru wa watu wetu, nchi yao ya Palestina.

Paraguay

Rais Mario Abdo Benítez alisema, “tunaungana na machungu ya kuondokewa na Papa mstaafu Benedict XVI, ambaye aliacha urithi wenye kuzaa matunda na kuonyesha maishani mwake kwamba imani, akili na haki vinaweza kwenda sambamba. Pumzika kwa amani.”

Mgombea urais nchini Paraguay, Efrain Alegre alisema, “pumzika kwa amani Benedict XVI. Papa mstaafu, hekima na ukuu wako mbele ya Kanisa utuambie kuhusu kiongozi mkuu na Mkristo.”

Ufilipino

Rais Bongbong Marcos alisema, “tuko katika huzuni kubwa baada ya kusikia kifo cha Papa Mstaafu Benedict XVI. Ufilipino ni mojawapo nchi zinazomwombea kwa ajili ya pumziko la milele la roho yake. Tunawaweka wapendwa wake katika sala zetu.

Askofu wa Kalookan Pablo Virgilio David, ambaye ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilipino, amemtaja papa wa zamani kama Papa wa upendo ambaye maaskofu wa Ufilipino watamkumbuka kwa furaha.”

Poland

Rais Andrzej Duda alisema, “Papa Benedikto XVI ameondoka kwenda kwenye nyumba ya baba. Ulimwengu umempoteza mmoja wa wanatheolojia mashuhuri wa karne ya 20 na 21, mshirika wa karibu wa Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili.

Rais Marcelo Rebelo de Sousa katika taarifa aliyoiandika kwenye tovuti ya Ofisi ya Rais wa Jamhuri kuwa Benedikto XVI atakumbukwa hususan katika kipindi chote cha miaka minane ya upapa wake.

Alisema alibaki kuwa kielelezo cha utulivu na utetezi wa tunu za Kanisa Katoliki, upendo kwa jirani, mshikamano na msaada kwa maskini zaidi na wasio na ulinzi, msamaha na upatanisho.

Rais huyo aliikumbuka ziara ya Kitume ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI nchini Ureno, Mei 2010.

“Wakati wa kuadhimisha miaka 10 ya kutangazwa wenyeheri Wachungaji Wadogo wa Fatima, Francisco na Jacinta Marto, bila kusahau maneno ya shukrani wakati huo aliyoonyeshwa kwa nchi yetu,” alisema.

Waziri Mkuu Antonio Costa anakumbuka kumpokea Benedict XVI mjini Lisbon alipokuwa bado Meya na anakumbuka kwamba kazi na kujitolea kwake kutasalia kuwa rejeo la waamini duniani kote.

Russia

Rais Vladimir Putin alimtaja Benedict XVI kama mtu mashuhuri wa kidini na mwanasiasa na mtetezi shupavu wa maadili ya jadi ya Kikristo.

Singapore

Rais Halimah Yacob, katika barua yake kwa Papa Francis, alisema amehuzunishwa sana kusikia kifo cha papa huyo wa zamani, na kuongeza kuwa, atakumbukwa na jumuiya ya Kikatoliki kwa michango yake ya kujitolea kwa imani ya Kikatoliki, kutetea malengo na maendeleo ya amani.

Waziri Mkuu Lee Hsien Loong, katika barua yake kwa Katibu Mkuu wa Jimbo la Vatican City, Pietro Parolin, alituma rambirambi zake za kina kwa niaba ya Serikali ya Singapore.

Afrika Kusini

Rais Cyril Ramaphosa alisema raia wote wa Afrika Kusini wanatafakari kwa makini uongozi wa roho Papa Benedict XVI alitoa kwa Kanisa lake na ubinadamu kwa upana zaidi.

Korea Kusini

Msemaji wa Chama Tawala cha People Power Party alitoa taarifa, akisema kujiuzulu kwa Benedict kulikuwa ishara ya ukarabati wa kanisa na uongozi wake na utakumbukwa milele.

Hispania

Mfalme Felipe VI alituma salamu zake za rambirambi kwa Papa Francis, akibainisha kuwa, alipokea habari kwa huzuni kubwa na kusisitiza urithi wenye matunda wa kiakili na kiroho ulioachwa na Benedict XVI.

Marekani

Rais Joe Biden alitoa taarifa akisema Papa Benedict XVI atakumbukwa kama mwanatheolojia mashuhuri, mwenye kujitolea kanisani maisha yake yote, akiongozwa na kanuni na imani yake.