Adaiwa kumuua mama yake mzazi kisa ndizi

Muktasari:

  • Kijana mmoja kutoka nchini Kenya amedaiwa kumuua mama yake mzazi baada ya kukuta amepika ndizi badala ya ugali, kisha naye kuuawa na wananchi.

Dar es Salaam. ‘Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni’ ndio unavyoweza kusema kutokana na kisa hiki cha mtoto kudaiwa kumuua mama yake mzazi, kisa hajapikiwa ugali.

 Maisha ya Magdalene Wangechi (68), yamekatishwa na mtoto wake, Patrick Irungu (36) baada ya kupika ndizi, jambo lililomkasirisha mtoto huyo aliyekuwa akitaka ugali.

Tovuti ya Tuko imeeleza tukio hilo limetokea Kijiji cha Gaturo, Kaunti ya Murang’a nchini Kenya.

Inadaiwa Irungu alianza kugombana na mama yake akimtaka ampatie ugali badala ya ndizi alizokuwa amepika.

Baada ya marumbano, inaelezwa Irungu alichukua panga na kumkata kichwa mama yake na kusababisha kifo.

Naibu Kamishna wa Kaunti ya Murang'a Kusini, Gitona Murungi amesema majirani walisikia wakati mama na mtoto huyo wakirushiana maneno.

"Majirani wamesema wakati ugomvi ukiendelea, baadaye walisikia mayowe, hali iliyowafanya waende eneo la tukio. Walipofika walimkuta mama huyo akiwa ameanguka chini huku damu zikimtoka na Irungu akiwa amesimama karibu naye," amesema Murungi.

Kamishna huyo amesema baada ya tukio hilo kijana huyo alitaka kukimbia, lakini majirani wakamkamata na wananchi wenye hasira waliendelea kumuadhibu na mwishowe alifariki dunia.

Imeandikwa na Sute Kamwelwe kwa msaada wa mashirika