Ajali ya ndege Nepal yaua 67, yatajwa kuwa ajali kubwa nchini humo
Muktasari:
- Watu 67 wamepioteza maisha nchini Nepal kufuatia ajali ya ndege iliyoanguka leo nchini humo ikiwa na abiria 72.
Dar es Salaam. Polisi nchini Nepal imethibitisha vifo vya watu 67 kufuatia ajali ya ndege iliyoanguka leo Januari 15, 2023 nchini humo ikiwa na abiria 72.
Ajali hiyo ya anga iliyotokea katika safu ya milima ya Himalaya imeripotiwa kuwa mbaya zaidi kushuhudiwa katika taifa hilo katika kipindi cha miongo mitatu.
“Tayari miili ya watu 31 imepelekwa Hospitali,” ofisa wa polisi nchini humo, Ak Chetri aliiambia Shirika la Habari la Ufaransa AFP. Ameongeza kwamba miili mingine 36 bado ilikuwa kwenye korongo la futi 600, eneo ambalo ndege hiyo ilitumbukia.
Hadi sasa hakuna taarifa rasmi za manusura wa ajali hiyo walioripotiwa, Msemaji wa Jeshi nchini Nepal, Krishna Prasad Bhandari aliiambia AFP.
Msemaji wa Shirika la Ndege la Yeti Airline la Nepal, Sudarshan Bartaula aliiambia AFP, miongoni mwa waliokuwemo kwenye ndege hiyo ni abiria 68 na wafanyakazi wanne
Kati ya hao, 15 walikuwa ni wageni, watu wenye asilia ya Asia watano, Warusi wanne na Wakorea wawili na wengine ni Wanepali.
Ofisa mmoja wa eneo hilo amesema baadhi ya walionusurika wamepelekwa hospitalini, hata hivyo taarifa hiyo haikuthibitishwa na Shirika la Ndege la Yeti Airlines.
Kwa mujibu wa AFP, video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ambazo zilionekana kupigwa baada tu ya ajali hiyo, zilionyesha miale ya moto inayowaka ardhini na moshi mweusi ukitoka angani.
Mei 2022, ajali ya ndege ilishuhudiwa nchini humo ambapo watu 22 walipoteza maisha katika ajali hiyo iliyohusisha ndege ya Shirika la Ndege la Tara Air.
Katika ajali hiyo Wanepali 16, watu wenye asili ya Asia wanne na Wajerumani wawili walipoteza maisha.