Atumia fedha za mkewe kuoa shoga wa mkewe

Nairobi. Wahenga walisema kikulacho kinguoni mwako. Usemi huu umemfika mwanamke mmoja wa Kenya aliyetambuliwa kwa jina moja la Mercy baada ya mumewe kuoa shoga yake.

Taarifa iliyotolewa na mtandao wa Tuko wa Kenya umebainisha kwamba licha ya usaliti huo, fedha zilizotumika kufanikisha ndoa hiyo ni za Mercy ambazo alikuwa akimtumia mumewe, mama huyo alipokuwa nje ya nchi.

Mercy ambaye ni mama wa watoto watatu amesema alikwenda kufanya kazi nje ya nchi na akiwa huko alikuwa akimtumia mumewe fedha kwa ajili ya kujenga nyumba na kuendesha miradi mbalimbali.

“Kumbe wakati natuma fedha zile kwa ajili ya ustawi wa familia yangu, mume wangu alikuwa anazitunza na akazitumia kumuoa rafiki yangu wa karibu,” amesema Mercy.

Mercy aliyefunga ndoa na mwanamume huyo miaka nane iliyopita amesema ametuma fedha kwa miaka mitatu kwa lengo la kununua ardhi na kujenga nyumba.

“Najisikia maumivu kwa sababu mshahara wangu nilimtumia lakini  amelipia mahari na kumuoa  rafiki yangu na sasa ameniacha na watoto hawa,” amesema.


Imeandaliwa na Pelagia Daniel