Auawa wakati akiamulia ugomvi wa wanandoa

Muktasari:

  • Mtu mmoja ameuawa wakati akiamulia ugomvi wa mume aliyekuwa akipigwa na mkewe huko Homa Bay nchini Kenya, Chifu wa eneo hilo amethibitisha.

Kenya. Jumatatu ya Machi 13, majira ya jioni ni siku ambayo Dan Ouma aliaga dunia baada ya kuamua kuingilia ugomvi kwa kusudi la kuwatenganisha wa wanandoa ambao mume alikuwa akipigwa na mke wake, tovuti ya Tuko imeripoti tukio hilo.

Matokeo yake Ouma mwenye umri wa miaka 24, alipigwa na kitu chenye ncha kali kichwani nyumbani kwa wanandoa huko Rachuonyo Kaskazini na baadae kumsababishia umauti baada ya kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa Bay hospitali.

 Akithibitisha kisa hicho, Chifu wa kata ya Kanyaluo Elius Ombim amesema kuwa mwanaume mmoja alikuwa akipigwa na mke wake na watoto kufuatia ugomvi wa kifamilia.

“Hili lilisababisha majirani akiwemo Ouma kuingilia kati lakini akawa ndiye aliyebeba msalaba wa vita hivyo,” amesema Ombim.

Ameendelea kusema kuwa Ouma alipigwa na kifaa kichwani na kukimbizwa hadi Hospitali ya Kadienge kabla ya kuhamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa Bay akiwa mahututi.

“Kwa bahati mbaya, aliaga dunia katika hospitali hiyo akipokea matibabu na mwili wake kuhamishiwa mochwari ya Homa Bay,” amesema.