Boris Johnson ataka Ukraine kusaidiwa kuipiga Urusi

Muktasari:

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amesema njia pekee ya kumaliza vita baina ya Ukraine na Urusi ni nchi ya Ukraine kushinda vita hiyo.



Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amesema njia pekee ya kumaliza vita baina ya Ukraine na Urusi ni nchi ya Ukraine kushinda vita hiyo.

Ametoa kauli hiyo nchini Ukraine baada ya kufanya ziara  na kubainisha kuwa ni upendeleo kwake kuonyesha mshikamano kwa nchi iliyo vitani.

Kiongozi huyo ambaye sasa anakumbana na maswali juu ya kiasi cha mali anazomiliki ameoneshwa katika taarifa za shirika la habari Aljazeera likibainisha kuwa picha zake zimeonekana  akiwa mji wa Boroddyanka eneo la Kyiv.

Johnson amesema mateso ya wananchi wa Ukraine yamedumu kwa kipindi kirefu.

"Njia pekee ya kumaliza mapigano haya ni Ukraine kushinda na kushinda inapaswa kuwa haraka iwekezakavyo. Huu ni wakati ambao tunapaswa kufanya mara mbili kuwapa Ukraine silaha wanazohitaji wamalize kazi haraka,” amesema Boris

Amesema siku zimekaribia kwa Rais wa Urusi,  Vladmir Putin kuanguka na itakuwa ni jambo la furaha kwa Taifa la Ukraine.

Julai mwaka 2022,  Boris  kabla ya kuachia nafasi ya uwaziri mkuu, Ikulu ya Kremlin mjini Moscow ilimkosoa kiongozi huyo aliyesimamia uungaji mkono thabiti wa Uingereza kwa Ukraine katika mapambano yake dhidi ya uvamizi wa Urusi.