China yaipiku Japan uuzaji magari nje
Muktasari:
Sekta ya magari China imepanuka katika miaka ya hivi karibuni kutokana na uwekezaji mkubwa katika magari ya umeme eneo ambalo makampuni ya Kijapani yamekuwa makini zaidi.
Tokyo, Japan/AFP. China imeipiku Japan kama muuzaji mkubwa zaidi wa magari duniani kwa mwaka 2023, takwimu kutoka kwa Jumuiya ya Watengenezaji Magari Japani (Jama) imeonyesha.
Sekta ya magari China imepanuka katika miaka ya hivi karibuni kutokana na uwekezaji mkubwa katika magari ya umeme, eneo ambalo makampuni ya Kijapani yamekuwa makini zaidi.
Japan ilisafirisha magari milioni 4.42 mwaka 2023, takwimu za Jama zimeonyesha, ikilinganishwa na magari milioni 4.91 yaliyouzwa nje na China.
Hata hivyo, ofisi ya forodha ya China imetangaza idadi kubwa zaidi kufikia magari milioni 5.22 yaliyouzwa, ikiwa ongezeko la asilimia 57 kwa mwaka hadi mwaka, huku gari moja kati ya matatu likiwa linalotumia umeme kikamilifu.
China ilikuwa tayari inasafirisha magari zaidi ya Japan kila mwezi, lakini takwimu za leo Jumatano Januari 31, zimethibitisha kuwa pia ilikuwa nambari moja kwa mwaka mzima.
Tofauti na wenzao wa China, watengenezaji magari wa Japan, ikiwa ni pamoja na kampuni ya Toyota, wamethibitisha kuwa ni kampuni kubwa zaidi duniani kwa mauzo ya vitengo, pia wanatengeneza magari mengi katika nchi nyingine.
Mwaka 2022, uzalishaji wa magari nchini Japan, bila kujumuisha pikipiki, ulifikia milioni 7.84, lakini uzalishaji wa nje wa nchi ulikuwa karibu milioni 17.
Badala ya miundo kamili ya umeme, watengenezaji magari wa Japan wameweka muundo unaotumia nguvu za betri za umeme na mfumo wa njia za kawaida.
Asilimia 1.7 pekee ya magari yaliyouzwa Japan mwaka wa 2022 yalikuwa ya umeme moja kwa moja, ikilinganishwa na karibu asilimia 15 katika Ulaya Magharibi, asilimia 5.3 Marekani na karibu moja kati ya matano (asilimia20) nchini China.
Watengenezaji magari wa Japan wameapa kurejea kwenye nafasi yao, huku Toyota ikilenga kuuza magari aina ya EV milioni 1.5 kila mwaka ifikapo 2026 na milioni 3.5 mwaka 2030.
Kampuni hiyo pia imewekeza kwa kiasi kikubwa katika teknolojia ya betri za kuhifadhi nguvu kubwa ya nishati na betri imara zaidi.
Teknolojia hii, ingawa haijathibitishwa hadi sasa, kwa kiwango kikubwa inamaanisha kuwa betri zitachaji haraka na kuyapa magari yanayotumia umeme uwezo mkubwa kuliko yale ya kawaida.
Kampuni ya China ya BYD mwezi huu ilinyakua taji la Tesla kwa mauzo mengi ya magari yote ya umeme, baada ya kupata msaada mkubwa wa Serikali ya China kwa sekta inayokua.
Mafanikio ya China katika magari ya umeme pia yameziweka kampuni zake mvutano, huku wadhibiti katika masoko ya Magharibi wakizishutumu kwa kukiuka masharti ya ushindani na kupanga bei isiyo ya soko.