Fahamu mwanajeshi aliyekosa usingizi kwa miaka 40

Muktasari:


  • Mwanajeshi Kern Paul kutoka Hungury hakuwahi kulala kwa miaka 40 baada ya kupigwa risasi kichwani wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia.

Usingizi ni moja kati ya vitu muhimu kwa binadamu. Ingawa baadhi ya watu hulala saa chache na wengine hulazimika kutumia vinywaji kama kahawa, ili kuwa macho muda mrefu, hii imekuwa tofauti kwa Kern Paul, mwanajeshi kutoka nchini Hungury ambaye hakuwahi kusinzia kwa miaka 40.

Stori hii inaanza miaka ya 1914, wakati dunia inaingia kwenye vita ya kwanza ya dunia iliyoibuka baada ya kuuawa kwa aliyekuwa kiongozi wa Austria, Archduke Franz Ferdinand na mke wake.

Kern, alikuwa mmoja kati ya wananchi waliojiunga na jeshi kwa ajili ya vita na akapangwa kwenye kikosi maalumu cha elite shock troop.

Kikosi hicho mara nyingi ndio huwa mstari wa mbele kwenye vita, hivyo askari wake huwa kwenye hatari ya kuuawa ama kupata majeraha makubwa.

Mwaka 1915 wakati wa mapambano na wanajeshi wa Russia, Kern alipigwa risasi ya kichwa iliyomsababishia majeraha hayo kiasi cha kutoweza tena kulala.

Baada ya kupelekwa hospitali ya Lemberg  kwa matibabu, baada ya vipimo daktari alieleza kwamba Kern anaweza kufariki ikiwa risasi itatolewa kwenye kichwa chake.

Kwa mujibu wa tovuti ya SOFREP, risasi hiyo iliingia kwenye fuvu la kichwa chake na kugusa sehemu ya ubongo iitwayo frontal lobe, ambayo huwa na kazi za hisia, kupanga na kutatua matatizo.

Kern alilazimika kurudi uraiani kutokana na tatizo hilo, lakini ajabu tangu wakati huo hakuwahi  kupata usingizi kwa miaka 40 hadi alipofariki dunia, licha ya kujilazimisha kufanya hivyo.

Kwa mujibu wanasayansi kutoka Marekani, muda mrefu ambao binadamu anaweza kukaa bila ya kulala ni saa 264 (sawa na siku 11), lakini kwa Kern inaonekana kuwa tofauti.

Mara nyingi ukikosa kulala unapata madhara mengi ikiwa pamoja na kupoteza kumbukumbu, kupata tabu ya kufikiria mambo, kuwa na kinga ndogo ya mwili, kuwa kwenye hatari ya kupata kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo, lakini Kern hakuathirika kabisa na hili kiasi cha madaktari kueleza huenda alikuwa akilala bila ya yeye kujua.

Kwa mujibu wa tovuti ya Sofrep, baadhi ya madaktari walidai ni ngumu mtu kukaa muda wote huo bila ya kulala na kuna uwezekano Kern alikuwa akilala mchana bila hata ya yeye kujua kama amelala.

Madokta wengine walisema mwanajeshi huyu alikuwa anatunga tu maneno. Kern anadaiwa alitembelea hospitali zote za madaktari waliokuwa wakisema maneno hayo ili wamfanyie vipimo na baada ya hapo waligundua kuwa ni kweli Kern hakuwa na uwezo wa kulala.

Alifariki dunia mwaka 1955 akiwa na umri wa miaka 71, jambo ambalo pia lilishangaza wataalamu wengi wa masuala wa afya kwa sababu moja ya matokeo ya mtu kutolala kwa muda mrefu ni kufariki mapema.