Hekaheka za Gen Z wakiandamana kuwakumbuka wenzao waliouawa Kenya

Muktasari:
- Maandamano ya leo Juni 25, 2025 ni kwa ajili ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu vijana maarufu GenZ kuuawa katika maandamnao yaliyofanyika mwaka jana.
Kenya. Mapema asubuhi ya leo Jumatano 25, 2025 vijana wa Kenya maarufu kama GenZ wameingia barabarani kufanya maandamano ya amani ikiwa ni kumbukumbu ya vifo vya wenzao waliofariki katika maandamano waliyoyafanya Juni, 2024.
Takriban watu 60 waliuawa mwaka jana na vikosi vya usalama katika wiki za maandamano ya kupinga ongezeko la ushuru na hali mbaya ya kiuchumi kwa vijana wa Kenya.
Kutokana na tukio hilo wanaharakati na familia za vijana waliouawa wametoa wito wa maandamano ya amani kuadhimisha ikiwa ni mwaka mmoja yalipotokea machafuko nchini humo.
Kwa mujibu wa tovuti ya Taifa Leo, asubuhi usalama ulikuwa umeimarishwa jijini Nairobi huku maofisa wa polisi wakifunga barabara kuu zinazoelekea katikati ya jiji hali iliyosababisha usumbufu kwa watumiaji wengine.

Hata hivyo, vijana hao wa GenZ walifanikiwa kupenya katikati ya jiji na kuanza maandamano, huku maduka yakifungwa na magari yakiwa machache tofauti na siku zingine.
Askari polisi waliendelea na doria huku wakikagua magari ingawa yale ya umma yakilazimika kushusha abiria mbali na katikati ya jiji na kuwalazimu wao kutembea kwa miguu.
Pia, Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, Kipchumba Murkomen ametembelea katikati ya Jiji la Nairobi, huku idara za usalama zikiongeza doria akiwa na Naibu Mkuu wa Polisi, Gilbert Masengeli.
Maandamano hayo pia yalianza kwa amani katikati mwa jiji la Nairobi huku nyimbo za kudai haki kwa waliouawa zikitawala.
Wakati huohuo kwa upande Mombasa maandamano ya amani yakiwa yameanza, waandamanaji walionekana wakibeba mabango yaliyoandikwa ujumbe wa kudai haki huku wakitembea kwa umoja bila vurugu.
Hata hivyo, kadri watu walivyoongezeka katikati mwa Jiji la Nairobi ndivyo maofisa wa usalama walivyoongezwa ili kuimarisha usalama.
Katika Kuanti ya Kisumu, maandamano hayo pia yalianza kwa amani huku waandamanaji wakidai haki kwa wale waliouawa mikononi mwa polisi. Maandamano hayo pia yaliendelea katika kaunti za Embu, Machakos, Uasin Gishu, Makueni, Nakuru, Nyeri, Kajiado na Kisii.
Mabomu yaanza kurindima
Baada ya muda milipuko ya mabomu ya machozi imeanza kusikika katikati ya jiji la Nairobi huku shughuli zote zikiwa zimesimama katikati ya miji na mitaa ambako wanaandamana.
Vijana na baadhi ya viongozi wa upinzani Kalonzo Musyoka, David Maraga na Eugene Wamalwa wameonrkana katikati ya jiji.
Mbunge wa Embakasa Mashariki Babu Owino na Seneta wa Busia pia wameonekana barabarani wakiungana na waandamanaji waliokuwa wakiimba nyimbo za kutaka haki.
Kwa mujibu wa Citizen Digital viongozi hao wa upinzani akiwemo Musyoka na Wamalwa wameikosoa vikali serikali kwa jinsi inavyoshughulikia maandamano, wakiishutumu kwa kukuza utamaduni wa kutokujali sheria, ghasia za serikali, na ukiukwaji wa katiba.
Wakizungumza na waandishi wa habari nje ya Kanisa Kuu la Holy Family Basilica leo asubuhi, viongozi hao wamethibitisha tena kuunga mkono maandamano yanayoendelea kutangaza mipango ya kuwakumbuka wale waliouawa wakati wa maandamano ya awali.
Kiongozi huyo wa chama cha Wiper pia amesema kuwa Juni 25 ni Siku ya Uwazi kwa Vijana, akipongeza ujasiri wa vijana wa Kenya wanaoendelea kudai uwajibikaji.
Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na kiongozi wa Chama cha Democratic Action Party (DAP-K) Eugene Wamalwa naye ameiishutumu serikali kwa kutawala kwa hofu.
"Kiwango hiki cha ulinzi kinaashiria utawala wenye hofu lakini kama upinzani wa wananchi, tunasimama na wananchi"
Aidha viongozi hao wamewalaumu wale wenye tabia ya uporaji wakati wa maandamano waksiema wanakosea na haipaswi kuwa hivyo.