ICJ yatupa kesi ya Ukraine dhidi ya Urusi

Muktasari:

  • Mahakama Kuu ya Umoja wa Mataifa ICJ, jana Jumatano imekataa madai ya Ukraine kwamba Urusi inafadhili ugaidi Mashariki mwa Ukraine.

The Hague. Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa na Ukraine ikiishutumu Urusi kwa kufadhili waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa nchi hiyo miaka 10 iliyopita.

Ukraine imeishutumu Moscow ikidai inafadhili watu wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine. Al Jazeera imeandika.

Imesema suala la uungaji mkono wake kwa waasi hao wanaounga mkono Urusi Mashariki mwa Ukraine ulikuwa ishara ya uvamizi kamili wa 2022.

Ukraine pia imetaka Urusi kuwafidia raia wote walionaswa kwenye mzozo huo pamoja na waathiriwa wa ndege ya shirika la ndege la Malaysia MH17, iliyodunguliwa mashariki mwa Ukraine Julai 17, 2014.

Jana Jumatano, Mahakama hiyo haikutoa uamuzi kuhusu madai ya Urusi kuhusika na kudungua ndege hiyo.

Vilevile, Mahakama hiyo imesema madai ya usambazaji wa silaha kwa makundi mbalimbali yenye silaha nchini Ukraine yapo nje ya upeo wa Mkataba wa Kimataifa wa Ufadhili Ugaidi (ICSFT).

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, Alexander Shulgin, Balozi wa Urusi nchini Uholanzi, ameishutumu Ukraine kwa kile alichokiita uongo wa wazi na mashtaka ya uwongo.

Naye, Mwanadiplomasia Mkuu wa Ukraine, Anton Korynevych amejibu kwamba Urusi ilikuwa inajaribu kuwafuta kwenye ramani.

"Kuanzia mwaka wa 2014, Urusi iliiteka Crimea kinyume cha sheria na kisha ikashiriki katika kampeni ya kufuta utamaduni, ikilenga watu wa kabila la Kiukreni na Tatars wa Crimea," Korynevych amesema.

Kesho Ijumaa, Februari 2, 2024 ICJ itatoa uamuzi katika kesi nyingine ambapo Ukraine imeishutumu Urusi kwa kutumia kimakosa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mauaji ya Kimbari ya 1948, ili kuhalalisha uvamizi wake wa Februari 24, 2022 nchini Ukraine.