Israel yadai kumuua kamanda wa makombora wa Hezbollah

Muktasari:

Hezbollah imekuwa ikirushiana risasi mara kwa mara na vikosi vya IsraelĀ tangu mshirika wake, kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas, kufanya shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa kusini mwa IsraelĀ Oktoba 7, 2023 na kusababisha vita huko Gaza.

Israel. Jeshi la Israel limesema shambulio la anga walilofanya nchini Lebanon jana Jumapili limemuua kamanda wa kitengo cha makombora cha Hezbollah.

Shambulizi hilo lililotua kwenye gari katika eneo la Kunin, limethibitishwa na Hezbollah kuwa kamanda huyo muhimu katika kitengo cha kupambana na vifaru cha vikosi vya Radwan, Ismail al-Zin alikuwepo ndani y gari hilo.

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant jana alizuru kamandi ya Jeshi la Kaskazini na kusema jeshi hilo litaendelea na operesheni zake dhidi ya Hezbollah.

Nchi hiyo ambayo ina hazina kubwa ya makombora, imekuwa ikirushiana risasi mara kwa mara na vikosi vya Israeli tangu mshirika wake kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas afanya shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa kusini mwa Israel, Oktoba 7, 2023 na kusababisha vita huko Gaza.

Mpaka sasa kutokana na mapigano hayo, watu wasiopungua 348 nchini Lebanon wameuawa, wengi wao wakiwa wapiganaji wa Hezbollah na raia takriban 68, kama linavyoripoti Shirika la utangazaji la AFP.

Inaelezwa mapigano hayo yameshasababisha makumi ya maelfu ya watu kuyahama makazi yao kusini mwa Lebanon na kaskazini mwa Israel, Jeshi linasema askari 10 na raia wanane pia wameuawa.

Kwingineko nchini Syria, idadi ya waliouawa katika mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya nchi hiyo inadaiwa kuongezeka hadi 52 wakiwamo wanajeshi 38 wa Serikali na wanachama kadhaa wa harakati za Hezbollah ya Lebanon.