Kenya yatumia mabilioni kulipa ada ya mikopo hewa

Dk Margaret Nyakang’o
Muktasari:
- Imeelezwa kuwa ada hiyo ya mkopo, ni ile ambayo Serikali ilimlipa mkopeshaji (benki) kama fidia ya kujitolea kwake kuutoa mkopo unaoombwa, na kwamba ada hizo huhusishwa sana na mikopo ambayo haijatolewa au kutumika.
Nairobi. Kati ya Julai 2022 na Septemba 2023,Serikali ya Kenya inadaiwa kutumia KSh1.89 bilioni (takriban Sh31.5 bilioni) kama ada ya mikopo hewa, ambayo nchi hiyo haijawahi kuipata, Mdhibiti wa Bajeti, Dk Margaret Nyakang’o amebainisha.
Mtandao wa Daily Nation, umeripoti hayo baada ya Dk Nyakang’o, akizungumza mbele ya Kamati ya Bunge ya Madeni na Ubinafsishaji, ambapo amesema fedha hizo ni pamoja na marejesho ya mikopo ya nje ya KSh499 milioni (takriban Sh8.2 bilioni).
Imeelezwa kuwa ada hiyo ya mkopo, ni ile ambayo Serikali ilimlipa mkopeshaji (benki) kama fidia ya kujitolea kwake kuutoa mkopo unaoombwa, na kwamba ada hizo huhusishwa sana na mikopo ambayo haijatolewa au kutumika.
Kwa maneno mengine, Mkopeshaji hulipwa fidia ya kutoa mkopo kwa kuwa ametenga pesa kwa ajili ya mkopeshwaji na kwamba hawezi kutoza riba.
Kwa upande mwingine, Dk Nyakang’o amewaambia wabunge hao kuwa kuna haja ya Hazina kuwa wazi katika usimamizi wa matumizi ya Mfuko Mkuu wa Huduma za Fedha (CFS), huku akisema Hazina inapaswa kuchapisha taarifa zaidi kuhusu matumizi ya CFS kama vile uchanganuzi wa gharama na miradi inayofadhiliwa na madeni.
"Kunapaswa kuwa na maelezo ya kwa nini bajeti ya CFS inayohusiana na mishahara, posho na huduma nyinginezo imeongezwa kwa kiasi kikubwa katika makadirio ya awali kisha kurekebishwa chini," Dk Nyakang'o amesema.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Kitui Kati, Makali Mulu; amesema kuna haja ya kujua ni wapi zimeenda fedha ambazo kila mwezi Wakenya wamekuwa wakilipa kama ada ya mkopo.
"Kwa kweli tunahitaji kujua kama nchi ambapo pesa hizi ambazo hatujawahi kuchukua au kutumia bado tunalipa ada yake. Tumeshangazwa kuwa baadhi ya mikopo hii imekuwepo tangu miaka 10 iliyopita,” Dk Makali amesema.
Pia mdhibiti huyo wa bajeti amedokeza kuwa, kwa utekelezaji mzuri wa bajeti, kodi unapaswa kwenda sambamba na kupunguza ukopaji na ujumuishaji wa fedha.
"Kwa kuzingatia viwango vya sasa vya deni la taifa, ukopaji mpya wa umma unapaswa kufanywa tu kwa miradi ambayo itaathiri vyema bajeti ya kitaifa," Dk Nyakang'o amewaambia wabunge.
Dk Nyakang’o alisisitiza haja ya kuangaliwa upya kwa sera za kiuhasibu za serikali ili kuhakikisha kunarekodi sahihi ya deni la taifa linalolingana na fedha zilizokopwa na miradi husika.
Alitoa wito kwa Hazina kupitia upya baadhi ya sera za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), akisema, nyingi zina athari mbaya katika utekelezaji wa bajeti ya nchi na uchumi.
"Hazina ya Kitaifa inafaa kufanya uhakiki wa kina wa sera hizi ili kulinda uchumi kutokana na athari mbaya," Dk Nyakang'o amesema.
Mdhibiti wa Bajeti pia alionya kuwa Mswada wa mishahara na pensheni umekuwa ukiongezeka, jambo ambalo, amesema, linahatarisha ukuaji wa uchumi.
Nyaraka zilizowasilishwa mbele ya kamati hiyo zinaonyesha kuwa, katika kipindi cha Julai na Novemba 2023, matumizi ya jumla yalikuwa KSh44.73 bilioni (takriban Sh737 bilioni)
"Hatua za stahiki zinapaswa kuchukuliwa ili kuharakisha ubadilishaji wa pensheni na malipo kutokana na faida iliyoainishwa dhidi ya mchango uliyobainishwa," Dk Nyakang'o alisema.
Katika azma ya kusimamia ipasavyo gharama kubwa za malipo ya deni la nje, Dk Nyakang’o amesema Serikali inatakiwa kuangalia upya sera ya sasa ya ukopaji ili kuandaa hatua za kuhakikisha uhimilivu wa deni hilo unadumishwa katika muda wa kati hadi mrefu.
Aidha, amesema, Serikali inapaswa kuzingatia urekebishaji wa deni la taifa na kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kufanya mapitio ya masharti ya ulipaji wa deni hilo.