Makamu wa Rais Gambia afariki dunia akiwa madarakani

Muktasari:

  • Makamu wa Rais wa Gambia, Badara Alieu Joof aliyekuwa na maoni yake ya kuwapendelea maskini serikalini, amefariki dunia nchini India, alipokuwa akipatiwa matibabu.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Gambia, Badara Alieu Joof amefariki dunia nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa kituo cha habari ‘The East African’ wameeleza kwamba kifo cha Joof kilithibitishwa katika taarifa ya leo Januari 18 na ofisi ya Rais huko Banjul.

"Kwa huzuni ninatangaza kuaga dunia Makamu wangu wa Rais, Mheshimiwa Badara Alieu Joof," taarifa hiyo imetolewa na Rais Adama Barrow kupitia ukurasa wake rasmi wa Facebook.

Joof ndiye Makamu wa Rais wa kwanza wa Gambia kufariki akiwa madarakani. Inasemekana aliugua ugonjwa kwa muda mfupi lakini hakujakuwa na habari kuhusu sababu kamili ya kifo chake.
Hata hivyo, tetesi za kuzidiwa zilianza kusambaa Desemba 2022.  Inaelezwa kwamba aliacha kuonekana hadharani muda mfupi baada ya kurejea kutoka katika ziara ya Jamhuri ya Uturuki.

Joof ambaye ni mwalimu kwa taaluma, aliwahi kuwa Waziri wa Elimu ya Juu katika utawala wa Barrow kuanzia Februari 22, 2017 hadi Mei 4, 2022 alipoteuliwa kuwa makamu wa rais kufuatia kuchaguliwa tena kwa Rais Barrow Desemba 2021.

Joof alikuwa maarufu miongoni mwa Wagambia wengi, hasa kutokana na maoni yake ya kuwapendelea maskini serikalini.
"Utumishi wa umma ni injini ya mawazo, injini ya programu (na) injini ya miradi. Pia watekelezaji wa miradi hiyo, programu na mawazo. Haiwezi kuwa biashara kama kawaida katika utumishi wa umma. kwa watu wa Gambia," alinukuliwa akisema katika taarifa yake maarufu wakati wa mkutano na watumishi wakuu wa serikali.