Makamu wa Rais wa Malawi akamatwa tuhuma za rushwa

Makamu wa Rais wa Malawi, Saulos Chilima

Muktasari:

  • Ofisi ya kupambana na rushwa nchini humo imesema kuwa kati ya Machi na Oktoba mwaka jana, Chilima alipokea zaidi ya dola 280,000 na vitu vingine kama malipo baada ya kusaidia kampuni mbili kupewa kandarasi za serikali.

Makamu wa Rais wa Malawi, Saulos Chilima amekamatwa kwa tuhuma za rushwa.

Ofisi ya kupambana na rushwa nchini humo imesema kuwa kati ya Machi na Oktoba mwaka jana, Chilima alipokea zaidi ya dola 280,000 na vitu vingine kama malipo baada ya kusaidia kampuni mbili kupewa kandarasi za serikali.

Taarifa kutoka kwa ofisi hiyo imesema Chilima atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka kadhaa yakiwemo makosa matatu ya ufisadi.

Awali Makamu huyo wa Rais alihojiwa na wachunguzi kutoka ofisi hiyo lakini hakuzungumzia madai hayo.


Chilima aligombea kiti cha urais mwaka 2019 lakini akashika nafasi ya tatu katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali.


Baadaye aliungana na Rais wa sasa Lazarus Chakwera kama mgombea mwenza. Lakini uhusiano wa hivi karibunu kati ya Makamu wa Rais na Rais Chakwera umezorota kutokana na shutuma za ufisadi na upendeleo serikalini.


Chilima amewahi kufanya kampeni katika jukwaa la kupinga ufisadi akiahidi kumaliza miongo kadhaa ya ufisadi serikalini na kumaliza umaskini katika mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani.