Mama wa watoto 7 ajiunga darasa la tatu

Ngelemo Leleruk ambaye ni mama wa watoto saba na mwanafunzi wa darasa la tatu

Muktasari:

  • Asema anataka maisha bora kwa familia yake kama ilivyo kwa marafiki zake aliosoma nao ambao wote wanamaisha mazuri, afichua kuwa mumewe na wanaye wanamuunga mkono.

Kenya. Mama wa watoto saba, Ngelemo Leleruk  ameishangaza dunia baada ya kuamua kujiunga darasa la tatu katika Shule ya Msingi ya Loikas iliyoko Kaunti ya Samburu baada ya kubaini kuwa marafiki zake wengi aliosoma nao wanamaisha bora.

Amesema ameazimia kupata elimu kwa namna yeyote ile na anatamani kubadilisha maisha ya familia yake kupitia elimu.

"Wenzangu wamesoma na wako mbele sana kimaisha, nimekuja kusoma na kupata maarifa kama wao," aliiambia Citizen TV Kenya.

Ngelemo mwenye umri wa miaka 31 alipoteza nafasi ya kusoma akiwa na umri mdogo baada ya kuolewa akiwa na miaka 13 na sasa katika miaka yake 18 ya ndoa, amezaa watoto saba ambao anawatunza na mume wake.

Mume wa Leleruk, Thomas Leleruk, alionyesha furaha yake na kuunga mkono mpango wa mke wake wa kurejea shuleni.

Mwalimu wake Rose Wamoyo, alimsifu Leleruk kwa ujasiri wake, "Ni mwanamke aliye na kiu cha elimu anauliza maswali na yuko tayari kusoma," amesema Wamoyo.

Leleruk, ambaye alitumia muda mwingi wa maisha yake kuchunga ng’ombe na kulea watoto wake, aliwahimiza wanawake kutafuta elimu.

"Napenda kuwasihi wanawake na akina mama, muhimu zaidi, wale ambao wako nyumbani na hawajasoma warudi shuleni wapate kazi na hata digrii," alisema.

Hadithi ya Leleruk imewagusa watu wengi mitandaoni huku wakimpongeza kwa hatua yake muhimu.