Mamlaka China kuchunguza vifo vya nguruwe

Muktasari:

  • Mamlaka za China zinachunguza nguruwe waliokufa na kukutwa kando ya mto, kwa mujibu wa ripoti ya vyombo vya habari inaelezwa kuwa jambo hilo linarudisha mwangaza juu ya usalama wa chakula na maji.

Mamlaka za China zinachunguza nguruwe waliokufa na kukutwa kando ya mto, kwa mujibu wa ripoti ya vyombo vya habari inaelezwa kuwa jambo hilo linarudisha mwangaza juu ya usalama wa chakula na maji.

Mizoga ya nguruwe iligunduliwa katika sehemu ya ndani ya Mongolia ya mto wa pili kwa urefu nchini humo na wengine walikuwa wameoza ndani ya maji, kwa mujibu wa Banyuetan, jarida linaloendeshwa na shirika la habari la serikali la Xinhua.

Mamlaka za serikali za mitaa zinachunguza chanzo cha vifo vya nguruwe hao na kuangalia kama walibeba ugonjwa wowote pamoja na kuua wadudu katika eneo hilo.

Hiyo siyo mara ya kwanza China kushuhudia nguruwe waliokufa katika mito yake. Mwaka 2013, maelfu ya nguruwe waliokufa waligunduliwa katika mto Huangpu huko Shanghai na  wengine waliripotiwa kuambukizwa na ugonjwa wa porcine circovirus ambao ulitishia kusambaa katika jimbo hilo.

Mwaka mmoja baadaye, mamlaka zilibaini nguruwe wengine zaidi ya 100 waliokufa kutoka Mto Ganjiang katika mji wa Nanchang.

Ugunduzi wa hivi karibuni umekuja wakati kundi la nguruwe likipona kutokana na uharibifu wa homa ya nguruwe. Ugonjwa huo ulizuka nchini humo mwaka 2018 na kuangamiza karibu nusu ya nguruwe katika nchi hiyo ambayo ni mzalishaji mkubwa wa nguruwe ulimwenguni.

Wasiwasi juu ya usalama wa chakula na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji wa nyama ya nguruwe umeongeza kasi ya kufungwa kwa mashamba madogo ya nguruwe kwa kutumia vifaa vikubwa na bora zaidi.