Marekani yakifungia Chuo Kikuu cha Harvard kudahili wanafunzi wa kigeni

Muktasari:
- Moja ya sababu kukifungia chuo hicho kinatuhumiwa kuchochea chuki dhidi ya Wayahudi, kushirikiana na Chama cha Kikomunisti cha China.
Washington. Marekani imetangaza kulifungia Chuo Kikuu cha Harvard kudahili wanafunzi wa kimataifa, huku ikiamuru wanafunzi wa kigeni walioko chuoni hapo kuhama mara moja au kukabiliana na hatari ya kupoteza hadhi yao ya kisheria ya kuishi nchini humo.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya chuo hicho maarufu kutuhumiwa kuchochea chuki na vurugu dhidi ya Wayahudi, pamoja na kile kinachoelezwa kuwa ni ushirikiano wa karibu na Chama cha Kikomunisti cha China (CCP), hali iliyozua taharuki katika masuala ya elimu na diplomasia.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Idara ya Usalama wa Ndani ya Marekani (DHS) imesema kuwa vitendo vya chuo hicho vinaenda kinyume na maadili ya kitaaluma na usalama wa taifa, hasa kwa kushindwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya matamko na matendo ya kibaguzi yaliyoripotiwa ndani ya kampasi.
“Tuna wajibu wa kuhakikisha taasisi za elimu haziwi sehemu ya kueneza chuki wala kuhusika na mashirika ya kigeni yenye agenda zisizo rafiki kwa Marekani,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Tuhuma dhidi ya Harvard zimekuja wakati ambapo kumekuwa na ongezeko la maandamano ya wanafunzi nchini humo, hasa yanayohusiana na mzozo wa Mashariki ya Kati. Ripoti zinaeleza kuwa baadhi ya mikutano ya wanafunzi na matamko ya kisiasa yamechukuliwa kuwa na mwelekeo wa kuunga mkono chuki dhidi ya Wayahudi.
Wanafunzi wa kimataifa waliopo chuoni hapo sasa wamepewa siku 60 kuhama kwenda vyuo vingine vilivyoidhinishwa, au waondoke nchini kwa hiari. Tayari baadhi ya mashirika ya kutetea haki za wahamiaji na wanafunzi wa kimataifa yamelalamikia uamuzi huo, wakisema ni wa ghafla na unaowaumiza wasiohusika.
Chuo Kikuu cha Harvard hakijatoa kauli rasmi kuhusu hatua hiyo, lakini taarifa za ndani zinasema uongozi wake unafanya mashauriano na mawakili pamoja na maofisa wa Serikali kutafuta suluhu kutokana na tuhuma hizo na maagizo yaliyotolewa.
Chuo Kikuu cha Harvard, kilichoanzishwa mwaka 1636 huko Cambridge, Massachusetts, ni moja ya vyuo vikuu vya zamani na maarufu zaidi duniani. Kilianzishwa na koloni la Massachusetts Bay na kilipewa jina la mwekezaji wake wa kwanza, John Harvard, ambaye alitoa maktaba yake binafsi na nusu ya mali yake kwa chuo hicho. Harvard imekuwa chuo maarufu duniani.
Chuo hicho kimekuwa kitovu cha elimu ya juu, tafiti za kisayansi, na maendeleo ya fikra duniani. Chuo hiki kinajivunia kuwa na vitivo mbalimbali kama vile Sheria, Tiba, Biashara, na Sayansi ya Siasa, na kimezalisha viongozi mashuhuri duniani wakiwemo marais wa Marekani na washindi wa Tuzo ya Nobel.