Mataifa matatu yatangaza kujiondoa ECOWAS


Muktasari:

  Nchi hizo ni Mali, Burkina Faso na Niger. Hata hivyo Ecowas yajibu ikisema iko tayari kwa mazungumzo

Dar es Salaam. Mataifa matatu ya Afrika Magharibi ya Mali, Burkina Faso na Niger, yametangaza kujiondoa katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS).


Mamlaka za nchi hizo zimetangaza uamuzi huo jana Jumapili Januari 28, 2024, huku zikishutumu umoja huo kukiuka itikadi zake hivyo kuwa tishio kwa nchi wanachama.


Ikumbukwe mataifa hayo yanaongozwa na viongozi wa kijeshi,  baada ya kushuhudiwa kwa mapinduzi ya serikali zao hivi karibuni ambapo mapinduzi yalifanyika nchini Niger Julai mwaka jana, Burkina Faso mwaka 2022 na Mali mwaka 2020.


Viongozi hao wa kijeshi wamesema katika taarifa yao ya pamoja iliyosomwa kwenye televisheni ya serikali katika nchi zote tatu,  kwamba ni uamuzi huru kujiondoa na jumuiya hiyo.


Hata hivyo,  kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, Jumuiya ilisema kwamba ina nia ya kutafuta suluhu ya mzozo wa kisiasa kwenye nchi hizo kwa kushinikiza kurejeshwa mapema kwa serikali za kiraia kupitia uchaguzi.

Aidha, nchi hizo ziliishutumu ECOWAS kwa kushindwa kuwasaidia kukabiliana na wapiganaji ambao waliingia Mali tangu 2012 na kisha kwenda Burkina Faso na Niger.


ECOWAS yasema haijapata taarifa

Hata hivyo, katika taarifa yake ya jana jumuiya hiyo ilisema kwamba iko tayari kwa ajili ya mazungumzo ili kupata suluhu baada ya hatua ya nchi hizo.

Lakini ilisema bado haijapokea taarifa rasmi ya moja kwa moja ya kujiondoa kwa mataifa hayo matatu.

Jumuiya hiyo yenye wanachama 15 ilianzishwa mwaka 1975 kwa ajili ya kukuza ushirikiano wa kiuchumi katika nchi wanachama, ambapo inachukuliwa kuwa mamlaka kuu ya kisiasa na kikanda ya Afrika Magharibi.


Umoja huo umekumbana na changamoto katika miaka ya hivi karibuni huku ikijitahidi kukabiliana na matukio ya mapinduzi katika ukanda huo.

ECOWAS ni jumuiya ambayo inatambua serikali za kidemokrasia pekee.