Mfalme Charles agundulika kuwa na saratani

Muktasari:

  • Mfalme Charles wa III mara ya mwisho alionekana hadharani juzi Jumapili kwenye ibada ya kanisa huko Sandringham.

Mfalme Charles III wa Uingereza amegundulika kuwa na saratani ambayo hata hivyo bado haijawekwa wazi, Kasri la Buckingham limetangaza.

Taarifa hiyo iliyotolewa usiku wa kuamkia leo Jumanne, Februari 6, 2024 na mwandishi wa habari za Familia ya Ufalme, Sean Coughlan imeeleza kuwa saratani hiyo imegunduliwa hivi karibuni wakati akipatiwa matibabu ya uvimbe katika tezi dume.

Hata hivyo, Kasri la Buckingham halijaweka wazi aina ya saratani hiyo, lakini kwa mujibu wa taarifa tayari Mfalme Charles ameanza matibabu jana Jumatatu.

Kasri la Buckingham linasema, “Ana mtazamo chanya juu ya matibabu yake na anatazamia kurejea kutekeleza kazi za umma haraka iwezekanavyo.”

Limeeleza kuwa Mfalme Charles ataahirisha shughuli zake kwa sasa na inatarajiwa wanafamilia wengine wakuu wa familia ya kifalme watamsaidia shughuli zake za umma wakati wa matibabu yake.

Ingawa atasitisha kutoa huduma Mfalme Charles (75) ataendelea na jukumu lake la kikatiba kama mkuu wa nchi.

Kabla ya taarifa za saratani, alifanyiwa upasuaji wa tezi dume katika hospitali ya kibinafsi ya London zaidi ya wiki moja iliyopita.

Mfalme aliweka wazi kuhusu matibabu yake ya tezi dume, kwa lengo la kuwahimiza wanaume kujitokeza kufanya uchunguzi.

Aina nyingi za saratani, nafasi ya kuipata huongezeka kadri umri unavyoongezeka. Takwimu za Uingereza zinaonyesha kwa wastani kila mwaka, zaidi ya theluthi (asilimia 36) ya wagonjwa wapya wa saratani ilikuwa watu wenye umri wa miaka 75 na zaidi.

Waziri Mkuu, Rishi Sunak amemtakia Mfalme Charles III apone haraka pamoja na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Labour, Sir Keir Starmer.

Charles, amekuwa mfalme baada ya kifo cha mama yake, Malkia Elizabeth II, Septemba 8, 2022,

Kuhusu saratani

Saratani hutokea wakati seli katika sehemu maalumu ya mwili hugawanyika kwa njia isiyoweza kudhibitiwa, seli zinazoweza kuenea kwa tishu nyngine za mwili pamoja na viungo.

Saratani ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanaendelea kusambaa na kuwapata wananchi wengi.

Kuongezeka kwa magonjwa ya saratani kunatajwa kunatokana na sababu mbalimbali, lakini zaidi mtindo wa maisha ambao huchochea kuzalishwa kwa seli rafiki zinazovutia kuibuka kwa magonjwa hayo.