Mgombea wa upinzani ashinda urais Liberia

Muktasari:

  • George Weah (57), amepoteza kibali cha kuongoza ungwe ya pili ya Taifa la Liberia kwa tofauti ya kura 28,000 dhidi ya Joseph Boakai (78) kupitia matokeo yaliyotangazwa jana.

Liberia. George Weah (57), amepoteza kibali cha kuongoza ungwe ya pili ya Taifa la Liberia kwa tofauti ya kura 28,000 dhidi ya Joseph Boakai (78) kupitia matokeo yaliyotangazwa jana.

 Katika matokeo yaliyotangazwa juzi Novemba 16, 2023 na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Boakai alishinda kwa asilimia 50.58 dhidi ya asilimia 49.42 za Weah kupitia wapiga kura 1,431, 388 waliojitokeza katika vituo 4,295 vya kupigia kura.

Hali ya shangwe iliibuka usiku wa kuamkia jana wakati matokeo ya uchaguzi huo yalipoonyesha mwelekeo wa kupatikana ushindi huo wa Boakai dhidi ya Weah aliyeweka heshima ya Taifa hilo na Afrika ya kuwa mwanasoka pekee Afrika kushindi Tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia mwaka 1995.

"Tuna kazi mbele yetu ya kufanya na ninafurahi kwamba raia wametupa kibali.Kwanza kabisa, tunataka kuwa na ujumbe wa amani na upatanisho,” amenukuliwa Boakai na Reuters muda mfupi baada ya matokeo kutangazwa.

Baada ya matokeo hayo, Weah kupitia hotuba yake amesema amempigia mshindani wake Boakai na kumpongeza kwa ushindi huo ulioweka historia ya kuendeleza ukuaji wa Demokrasia nchini humo.

Weah amesema ataachia nafasi hiyo kwa amani huku akiwataka wafuasi wake wakubaliane na matokeo ya ushindi wa Boakai aliyemshinda uchaguzi wa mwaka 2017 kwa asilimia 62 ya kura zote. 

"Muda mchache uliopita nimezungumza na Rais aliyechaguliwa Joseph Boakai na kumpongeza kwa ushindi. Nawaomba wote kufuata mfano wangu na kukubaliana na matokeo," amesema Weah.

Boakai ni amewahi kuwa Waziri wa Kilimo miaka ya 1980 nchini humo.

Weah amefanya nini?

Liberia inajitahidi kujikwamua katika athari za kiuchumi baada ya vita viwili vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoua zaidi ya watu 250,000 katika mwaka 1989 hadi 2003 kabla ya janga la Ebola la 2013/16.

Wadadisi wa duru za kisiasa wanasema Weah aliingia Ikulu baada ya kujenga heshima ya Taifa hilo duniani kupitia umaarufu wake kwenye soka na uzoefu wake katika siasa za kimataifa.

Baada ya kuingia Ikulu mwaka 2018, mwanasoka huyo maarufu aliongoza taifa hilo kwa miaka sita baada ya kuikuta ikiwa inakabiliwa na changamoto nyingi za sekta ya afya, elimu na miundombinu.

Aliwaahidi Walaiberia kuwaondoa pia katika hali mbaya ya umaskini na kukuza uchumi wa taifa hilo.

Uchambuzi wa mashirika mbalimbali ya vyombo vya habari umenukuu changamoto ya Weah kutofanikiwa kupunguza vitendo vya rushwa, biashara na matumizi ya dawa za kulevya.