Mpango wa UK kuwahamishia Rwanda wakimbizi wapingwa
Muktasari:
- Mpango huo kwa mara ya kwanza ulitangazwa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, akisema watatumia dola milioni 160 na kwamba utaokoa maisha ya wahamiaji wengi ambao mara nyingi hujikuta kwenye mikono ya wasafirishaji haramu.
Dar es Salaam. Mahakama ya juu nchini Uingereza, imeupinga mpango wa Serikali ya nchi hiyo wa kuwahamishia Rwanda, wakimbizi walioingia nchini humo, ikisema ni kinyume cha sheria.
BBC imeripoti kuwa katika hukumu ya Hakimu Lord Reed, imeonekana kuwa mpango huo ungeweza kutumiwa kuwaondoa wakimbizi wa kweli na hivyo kuwaweka katika hatari ya kurudishwa katika nchi walizokimbia.
Uamuzi huo utatolewa baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani kuwasilisha rufaa kupinga uamuzi wa awali wa Mahakama ya Rufaa uliobainisha kuwa mpango wa kuwahamishia Rwanda waomba hifadhi wa Uingereza, kinyume cha sheria.
"Jaribio la kisheria ambalo linapaswa kutumika katika kesi hii ni kama kuna sababu kubwa za kuamini kwamba wanaotafuta hifadhi na wakapelekwa Rwanda, watakuwa katika hatari ya kurudishwa tena katika nchi zao,” amesema na kuongeza;
"Kwa mujibu wa ushahidi nilionao, Mahakama ya Rufaa iliamuru kuwa kulikuwa na sababu hizo. Maoni yetu ni kuwa walikuwa na haki ya kufikia uamuzi huo. Hakika, baada ya kuchukuliwa kwa ushahidi wenyewe, tunakubaliana na uamuzi huo.”
Hakimu huyo aliendelea kueleza: “Tunakubali maoni ya Waziri wa Mambo ya Ndani kwamba Serikali ya Rwanda iliingia mkataba huo kwa nia njema, na kwamba uwezo wa mfumo wa Rwanda wa kutoa maamuzi sahihi na ya haki unaweza kujengeka na utajengeka.”
"Lakini, tukijiuliza kama kulikuwa na sababu kubwa za kuamini kuwa hatari hiyo ya kurudishwa walikotoka kama ilikuwepo wakati huo, tumehitimisha kuwa ilikuwepo. Mabadiliko yanayohitajika ili kuondoa hatari ya kurudishwa tena yanaweza kutolewa katika siku zijazo, lakini hayajaonyeshwa kuwa yapo sasa,” amesema.
Serikali ya Rwanda yajibu
Dakika chache baada ya uamuzi huo, Serikali ya Rwanda imetoa tamko ikisema "haijafurahia" kutajwa kama eneo ambalo sio nchi ya tatu iliyo salama.
Taarifa hiyo ya Rwanda imesema: "...huu ni uamuzi unaotokana na na mfumo wa mahakama wa Uingereza. Hata hivyo, tunapingana na uamuzi kwamba Rwanda sio nchi ya tatu salama kwa wanaotafuta hifadhi na wakimbizi.”
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: “Rwanda na Uingereza zimekuwa zikifanya kazi pamoja ili kuhakikisha kuunganishwa kwa waomba hifadhi waliohamishwa katika jamii ya Rwanda, ambayo imejitolea kutekeleza majukumu yake ya kimataifa, na tumetambuliwa na UNHCR na taasisi nyingine za kimataifa kwa jinsi tunavyowashughulikia wakimbizi.”
"Katika mchakato huu wa kisheria tumekuwa na shughuli nyingi kuendelea kutoa maendeleo kwa Wanyarwanda, na kufanya kazi pamoja na washirika wa kimataifa kutatua baadhi ya changamoto kubwa ambazo Afrika na dunia nzima inakabiliana nazo. Tunachukulia kwa uzito mkubwa majukumu yetu ya kibinadamu, na tutaendelea kuyatekeleza,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Mpango huo wa Serikali umekuwa ukipingwa vikali na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu, wanaodai Rwanda haiwezi kuwa nchi salama kwa wakimbizi na wahamiaji hao
Kwa mujibu wa mtandao wa UN News, mwezi Juni mwaka jana, Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi. Alionekana kupinga mpango huo huku akisisitiza kuwa Uingereza imetia Saini mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi na kwamba “kujaribu ‘kuuza’ nje ya nchi wajibu uliomo kwenye mkataba huo ni kinyume na azma yoyote ya kimataifa ya kusaidiana majukumu.”
Rwanda ilikuwa na historia ya kipekee ya kukaribisha na kusaidia maelfu ya wakimbizi kutoka DRC na Burundi, alisema Grandi akiongeza kuwa nchi hiyo haina uwezo na miundombinu ya kuhudumia wakimbizi kwa kuzingatia mahitaji ya sasa.
“Ingekuwa ni kutoka Rwanda kwenda Uingereza, pengine tungaliweza kujadili, lakini hapa tunazungumzia, Uingereza, nchi ambayo ina mifumo na inahamishia jukumu lake kwa nchi nyingine, Rwanda,” alisema.
Grandi alitupilia mbali madai ya Uingereza kuwa mpango huo ulikuwa na lengo la kuokoa watu kutoka safari hatarishi za boti kupitia njia ya majini ya Uingereza kutoka pwani ya Ulaya.
“Namaanisha kuokoa watu kutoka safari hatarishi ni jambo muhimu sana,” alisema Grandi, lakini “je hii ni njia sahihi? Ni sababu ya msingi ya hatua hii kweli, mimi sidhani.”
Ametaka mawasiliano zaidi na Ufaransa ambako ndio wanatoka wakimbizi wengi zaidi watakaoathiriwa na mpango huu wa kuwapelekea Rwanda watu walioomba hifadhi nchini Uingereza, akisema “Ufaransa ina mifumo ya kusaidia wakimbizi hifadhi.”
Mpango huo kwa mara ya kwanza ulitangazwa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, akisema watatumia dola milioni 160 na kwamba utaokoa maisha ya wengi wa wahamiaji ambao mara nyingi hujikuta kwenye mikono ya wasafirishaji haramu.