Mtoto wa Bongo ashitakiwa kwa tuhuma za rushwa

Mtoto wa Rais wa Gabon aliyepinduliwa, Ali Bongo Ondimba

Libreville. Mtoto wa Rais wa Gabon aliyepinduliwa, Ali Bongo Ondimba na washirika kadhaa wameshtakiwa kwa ufisadi na kuwekwa kizuizini, mwendesha mashtaka wa Serikali ameiambia AFP leo Septemba 20, 2023.

Mtoto mkubwa wa Bongo, Noureddin Bongo na msemaji wa zamani wa Rais, Jessye Ella Ekogha pamoja na watu wengine wanne wa karibu na kiongozi aliyeondolewa madarakani, “wameshtakiwa na kuwekwa kizuizini kwa muda” jana Jumanne, alisema mwendesha mashtaka wa Serikali, Andre-Patrick Roponat.

Bongo (64) ambaye alitawala nchi hiyo ya Afrika ya Kati yenye utajiri wa mafuta tangu 2009, alipinduliwa na viongozi wa kijeshi Agosti 30, 2023, muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi wa Rais.

Matokeo hayo yalitajwa kuwa ya udanganyifu na upinzani na viongozi wa mapinduzi ya kijeshi, ambao pia wameutuhumu utawala wake kwa ufisadi ulioenea na utawala mbaya.

Siku hiyo hiyo ya mapinduzi, askari walimkamata mtoto mmoja wa Bongo na maofisa watano waandamizi wa Baraza la Mawaziri.

Televisheni ya kitaifa ilionyesha picha za watu waliokamatwa mbele ya masanduku yaliyojazwa pesa zinazodaiwa kukamatwa kutoka kwenye nyumba zao.

Baada ya mapinduzi, mke wa Bongo, Sylvia Bongo aliwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani katika mji mkuu Libreville “kwa usalama wake”, kwa mujibu wa mamlaka.