Mtoto wa miaka 12 aua, ajeruhi kwa bastola

Muktasari:

 Mwanafunzi mmoja amefariki dunia na wengine wawili wamejeruhiwa baada ya mwenzao mwenye umri wa miaka 12 kufyatua risasi katika shule ya msingi Finland

Finland. Mwanafunzi mmoja amefariki dunia na wengine wawili wakijeruhiwa baada ya mwenzao mwenye umri wa miaka 12 kufyatua risasi katika shule ya msingi nchini Finland.

Tukio hilo limetokea leo Aprili 2, 2024 katika shule hiyo ya Viertola huko Vantaa, kitongoji cha Helsinki yenye jumla ya wanafunzi 800 na wafanyakazi 90.

Inaelezwa kuwa, mtoto huyo alienda shule na bastola kisha kuanza kufyatua risasi.

Mkuu wa Polisi Ilkka Koskimäki kutoka Idara ya Polisi ya Mashariki amewaambia waandishi wa habari mmoja wa wanafunzi alikufa papo hapo baada ya kupigwa risasi.

Pia, polisi wamethibitisha tukio hilo huku wakitangaza kumkamata mtoto huyo muda mfupi baada ya kutenda kosa hilo na kujaribu kukimbia alipowaona polisi wanakuja, EuroNews imeripoti.

Taarifa zaidi zinasema majeruhi ambao wana umri sawa na mshambuliaji huyo, wamekimbizwa hospitalini japokuwa hawajatambulika kwa urahisi.

Mtoto huyo kwa sasa amewekwa chini ya uangalizi wa maofisa wa ustawi wa jamii kwa kuwa umri wa chini wa uhalifu nchini humo ni miaka 15, kwa sasa mshukiwa hawezi kukamatwa rasmi.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Finland Mari Rantanen ameandika kwenye X, (zamani Twitter) kuwa siku ya leo imeanza vibaya na kwa kuogofya.

"Kumekuwa na tukio la kupigwa risasi katika Shule ya Viertola huko Vantaa. Ninaweza kufikiria tu uchungu na wasiwasi ambao familia nyingi zinapitia kwa sasa," ameandika.

Mathalani, Rais wa nchi hiyo, Alexander Stubb na Waziri Mkuu Petteri Orpo wametoa salamu za rambirambi kwa familia za waathiriwa kwenye chapisho la X huku wote wakisema wameshangazwa na tukio hilo.

"Kinachofanya kushtua ni umri wa mwathiriwa na mshukiwa, lakini nawahakikishia hili litapita na halitajirudia tena," Orpo amesema wakati wa mkutano na wanahabari. Kwa sasa uchunguzi wa mauaji hayo unaendelea.

Ikumbukwe, Septemba 2008, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 22 aliwapiga risasi na kuwaua watu 10 kwa kutumia bastola katika chuo cha ufundi huko Kauhajoki, Kusini Magharibi mwa Finland, kabla ya kujipiga risasi.

Katika Taifa hilo lenye watu milioni 5.6, kuna zaidi ya bunduki milioni 1.5 zenye leseni na wamiliki wa leseni wapatao 430,000, kulingana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Finland.

(Imeandaliwa na Sute Kamwelwe)