Mwanajeshi aomba ugali kizimbani apate nguvu kujibu mashtaka

Muktasari:

  • Mwanajeshi mmoja ambaye anashikiliwa kwa tuhuma za kumpiga na kumjeruhi raia, ametoa mpya mahakamani baada ya kumuomba hakimu ugali ale ili apate nguvu ya kujibu mashtaka yanayomkabili.

Kenya. Japhet Olindo ambaye ni mwanajeshi wa Kenya alichekesha umma uliofika mahakamani Eldoret jana Jumatatu, alipomlilia hakimu akimuomba apewe ugali ale ili apate nguvu ya kujibu mashtaka, tovuti ya Taifa Leo imeripoti kisa hicho.

“Mheshimiwa, kabla sijasomewa mashtaka naomba uninunulie ugali, nina njaa sana sijapewa chakula tangu niwekwe selo, ninakaribia kuzimia tafadhali fanya jambo kabla sijaanza kushtakiwa,” alisema Olindo.

Ilibidi hakimu Keynes Odhiambo aweze kumbembeleza na kuahidi kumnunulia ugali, ndipo akakubali kujibu shtaka lake la kumjeruhi mtu.

“Nimesikia kilio chako kwa leo nitakununulia ugali kabla hujaondoka hapa kortini jibu shtaka kwanza na mimi nitatimiza ahadi yangu,” alimuahidi Odhiambo.

Vilevile Olindo alimwambia hakimu huyo mwandamizi mkuu kuwa anahofia endapo akipewa dhamana asiyoweza kuimudu, huenda mkewe akachukuliwa na wanaume wengine akiwa mahabusu (korokoroni).