Ndege mbili zagongana angani

Muktasari:

  • Ndege mbili zimegongana na kuanguka kwenye maonyesho ya anga katika jimbo la Texas nchini Marekani.

Dar es Salaam. Ndege mbili zimegongana na kuanguka kwenye maonyesho ya anga katika jimbo la Texas nchini Marekani.

Ndege hizo za zamani za Vita vya Pili vya Dunia (WWII), moja ya Boeing B-17 Flying Fortress na P-63 Kingcobra zilikuwa zikishiriki katika maonyesho ya anga karibu na Dallas jana Jumamosi 12, 2022.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa, bado haijabainika kuwa ndege hizo zilikuwa na watu wangapi, ingawa baada ya kugongana zilianguka na kuwaka moto.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini humo imesema itachunguza ajali hiyo katika Onyesho la Ndege la Wings Over Dallas, ambalo linajieleza kuwa onyesho la kwanza la anga la WWII la Marekani.

Tukio hilo la siku tatu lilikuwa likifanyika kwa heshima ya Siku ya maveterani na kati ya watu 4,000 na 6,000 walikuwa wakitazama onyesho hilo.

Meya wa Dallas, Eric Johnson amesema idadi ya waliojeruhiwa bado haijathibitishwa.