Ndege ya kivita ya Urusi yashambulia kwa bahati mbaya mji wake

Muktasari:

  • Ndege ya kivita ya Urusi imeshambulia kwa bahati mbaya mji wa Belgorod ulioko karibu na mpaka wa Ukraine na kujeruhi watu watatu. 

Moscow. Wizara ya Ulinzi mjini Moscow imesema ndege ya kivita ya Urusi ilishambulia kwa bahati mbaya mji wa Belgorod karibu na mpaka na Ukraine.

Gavana wa eneo hilo Vyacheslav Gladkov amesema mlipuko huo umeacha shimo kubwa lenye upana wa takriban mita 20 (futi 60) katikati mwa jiji.

Gladkov amesema watu watatu walijeruhiwa na majengo kadhaa kuharibiwa.

Ndege ya kivita aina ya Su-34 ilirusha bomu hilo kwa bahati mbaya, wizara imesema.

Wizara ya Ulinzi imesema kuwa bomu hilo lilianguka saa 22:15 saa za Urusi jana Alhamisi.

Bomu hilo lilitua kwenye makutano ya barabara mbili karibu na katikati ya jiji na karibu na majengo ya makazi.

Gladkov amesema wanawake wawili walipelekwa hospitalini kwa matibabu na jengo la ghorofa tisa liliharibiwa.

Picha na video kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha nyumba zilivyoharibiwa na mlipuko huo, na gari moja likiwa juu ya paa la duka la karibu na jengo la ghorofa sababu ya mlipuko huo.

Jiji la Belgorod liko karibu maili 25 (kilomita 40) kutoka mpaka wa Ukrain kaskazini mwa mji wa pili kwa ukubwa wa Ukraine, Kharkiv, na watu katika mji huo wamekuwa wakiishi kwa hofu ya mashambulizi ya makombora ya Ukraine tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwaka jana.