Niger yawatimua mabalozi wa nchi nne ikiwemo Ufaransa
Muktasari:
- Viongozi wa kijeshi wa Niger wametoa saa 48 kwa mabalozi wa Ufaransa, Ujerumani, Nigeria na Marekani, kuondoka nchini humo, wakati mvutano ukizidi kuongezeka kuhusu tishio la hatua za kijeshi kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (Ecowas).
Dar es Salaam. Viongozi wa kijeshi wa Niger wametoa saa 48 kwa mabalozi wa Ufaransa, Ujerumani, Nigeria na Marekani, kuondoka nchini humo, wakati mvutano ukizidi kuongezeka kuhusu tishio la hatua za kijeshi kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (Ecowas).
Mtandao wa DW umeandika kuwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Niger, imeziandikia barua tofauti nchi hizo ikisema uamuzi huo umetokana na hatua ya mabalozi wa nchi hizo kukataa mwaliko wa Serikali kwa ajili ya mkutano wa jana Ijumaa, lakini pia kutokana na serikali zao hizo kuwa kinyume na maslahi ya Niger.
Hata hivyo Ubalozi wa Ufaransa nchini Niger umelikataa tangazo hilo ukisema kuwa Paris, hautambui mamlaka ya watawala wa kijeshi.
Ufaransa imeunga mkono mara kwa mara wito wa Ecowas wa kutaka kurejeshwa madarakani kwa rais Mohamed Bazoum, ambaye alipinduliwa Julai 26, mwaka huu.
Jana jioni Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa ilieleza kuwa, "wapinzani hawana mamlaka ya kufanya ombi hili, kibali cha balozi kinakuja tu kutoka kwa mamlaka halali zilizochaguliwa za Niger."
Ufaransa inao wanajeshi 1,500 walioko Niger ambao walikuwa wakimsaidia Bazoum katika vita dhidi ya wanamgambo ambao wanaendesha uasi wao nchini humo kwa miaka mingi, huku Marekani ikiwa na takriban wanajeshi elfu moja nchini humo.
Mapema Ijumaa, Ecowas iliwataka viongozi wa mapinduzi wa Niger kufikiria upya msimamo wao na kushinikiza kurejeshwa kwa utawala wa kiraia, huku tishio la nguvu likiwa bado ‘mezani.”
Viongozi wa kijeshi wa Niger pia wameonya dhidi ya uingiliaji kati wowote, wakishutumu Ecowas kushirikiana na nchi ya kigeni ambayo haikutajwa jina.
Siku ya Alhamisi Agosti 24, 2023; nchi hiyo ilikubaliana na serikali za nchi jirani za Mali na Burkina Faso kuruhusu wanajeshi wake kuingia katika ardhi ya Niger endapo kutakuwa na jaribio lolote la kichokozi.
Kwa mantiki hiyo, sasa jeshi la Niger limeunda muungano wa kijeshi na nchi jirani za Burkina Faso na Mali ambazo watawala wake pia walichukua madaraka kwa njia ya Mapinduzi.
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo tatu walikutana mjini Niamey ili kujadili ushirikiano zaidi wa kiusalama pamoja na masuala mengine.
Burkina Faso na Mali zimesisitiza msimamo wao wa kukataa uingiliaji wowote wa kijeshi dhidi ya Niger ukiutaja kama tangazo la vita dhidi yao.
Ecowas imekuwa ikijaribu kufanya majadiliano na viongozi wa mapinduzi lakini imeonya kwamba iko tayari kupeleka wanajeshi nchini humo kwa lengo la kurejesha utulivu ikiwa juhudi za diplomasia zitashindikana.
Mazungumzo kati ya Ecowas na utawala wa kijeshi wa Niger yalifanyika mwisho mwa wiki iliyopita. Makubaliano hayo yaliyotangazwa Alhamisi pia yanawataka watatu hao kuchukua hatua za pamoja dhidi ya makundi ya kigaidi yanayoendesha oparasheni zao huko na pia kulinda mipaka yao.
Kwa miaka mingi, nchi za ukanda wa Sahel zimekuwa zikitishiwa na wanamgambo mbalimbali wa kigaidi, huku baadhi yao wakifungamanishwa na makundi ya Al-Qaeda na Dola ya Kiislamu.
Wakati hayo yakijiri, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron jana Alhamisi ametoa wito wa kurejea kwa utaratibu wa kidemokrasia na kuachiliwa kwa Rais Mohamed Bazoum, Mahusiano kati ya Ufaransa na Niger yamedorora tangu yalipofanyika mapinduzi ya kijeshi nchini Niger.
Pamoja na uwepo wa jeshi la Ufaransa katika ukanda huo, Rais Macron ameeleza kwamba bado ukanda wa nchi za Afrika magharibi hazijaonyesha nia ya kushirikiana ipasavyo na hivyo kubaki nyuma.
Kwa upande mwingine, mataifa jirani kama algeria yamejitokeza kupinga tishio la Ecowas kutuma kikosi cha kijeshi kuingilia kati iwapo utawala mpya wa kijeshi utashindwa kurejesha utawala wa demokrasia na kwamba bado ipo nafasi ya mazungumzo ya kidiplomasia.
Mapinduzi ya kijeshi nchini Niger yalipata ungwaji mkono mkubwa wa raia nchini humo na wakati nchi za Burkina Faso na Mali zikionesha kuunga mkono kinachoendelea, raia nchini humo pia waanamini kundi la mamluki la Wagner licha ya kudaiwa kufariki kwa kiongozi wake Yevgeny Prighozhin bado waanamini kundi hilo litawasaidia kukabiliana na ushawishi wa mataifa ya magharibi.
"Tunaomba kwamba Mwenyezi Mungu aimarishe uhusiano na (Wagner) ili kuendeleza mpango huo. Ikiwa uhusiano huo ni mzuri na wenye nguvu inawezekana wataendelea na mpango huo hata baada ya kifo chake (Yevgeny Prigozhin).”
Niger yenye idadi ya wakaazi karibu milioni 26 ni moja ya nchi maskini zaidi duniani na chini ya utawala wa Mohammed Bazoum, Niger ilikuwa inatazamwa kuwa moja ya washirika wa mwisho wa kimkakati wa nchi za Magharibi katika mapambano dhidi ya ugaidi katika ukanda wa Sahel.