Njiwa kutoka Marekani anusurika kifo Australia

Canberra. Lebo bandia imemnusuru na kifo njiwa aliyetakiwa kuuawa nchini Australia baada ya kuripotiwa kutokea Marekani na kuingia katika nchi hiyo ambayo imeweka sheria kali ya kutotoka nje ili kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19.

Njiwa huyo anayefahamika kwa jina la Joe alitakiwa kuuawa kwa kuwa amekiuka masharti dhidi ya Covid-19 lakini baada ya uchunguzi maofisa wa Australia wamemkuta na lebo feki, hivyo kutilia shaka asili yake.

Joe alivuma katika vyombo vya habari duniani baada ya kukutwa katika bustani huko Melbourne akiwa amevaa lebo ambayo inamtambulisha kuwa Mmarekani lakini mamlaka za Australia zimeeleza kuwa huenda ndege huyo ni wa nchini humo.

“Kufuatia uchunguzi ambao ulifanywa, wamebaini kuwa njiwa huyo Joe anawezekana kuwa asili yake ni Australia na hawezi kuwa hatari kwa maambukizi,” idara ya kilimo, maji na mazingira imetangaza Ijumaa.

Idara hiyo imejiridhisha kuwa lebo aliyokuwa nayo ndege huyo mguuni ni feki na taarifa zaidi zinaeleza kuwa hakuna hatua kali itakayochukuliwa dhidi ya ndege huyo.

Mkazi wa Melbourne Kevin Celli-Bird alikieleza chombo kimoja cha habari kuwa walimkuta ndege huyo nyuma ya bustani Desemba 26. “Alionekana kuwa na njaa kali hivyo nilimpelekea biskuti”.

Ndege huyo aliripotiwa kupotea wakati wa mashindano huko Oregon, Marekani mwishoni mwa mwezi Oktoba, na akaonekana miezi miwili baadaye katika mji wa Melbourne .

Joe alikuwa hajakamatwa bado lakini mamlaka za Austaralia zilisema auawe kwa sababu anaweza kuambukiza ndege wengine.

”Suala ambalo linawezekana kufanyika ili kudhibiti hatari ya maambukizi ni kumuua ndege huyo”.