NMG yaeleza mikakati kukabili mabadiliko ya tabianchi

Muktasari:

Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Nation Media Group (NMG), Dk Wilfred Kiboro, amesema kupitia vyombo vya habari inavyomiliki watatoa elimu mabadiliko ya tabia nchi na tutaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuchagiza ajenda hiyo.

Nairobi. Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Nation Media Group (NMG) inayomiliki kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Dk Wilfred Kiboro amesema kampuni hiyo kupitia vyombo vya habari inavyovimiliki itaendelea kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kutoa elimu na kuanzisha mijadala ya kutoa suluhu.


Kauli hiyo ameitoa leo Alhamisi Desemba 8, 2022 akizungumza kwenye tamasha la ‘Kusi Ideas Festival’ lililoandaliwa na kampuni hiyo linalofanyika Nairobi nchini Kenya.


“Kupitia vyombo vyetu vya habari ambavyo tunavimiliki (magazeti, redio na televisheni) tutaendelea kutoa elimu hiyo (mabadiliko ya tabia nchi) na tutaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuchagiza ajenda hii ili iwafikie wananchi wengi,” amesema.

Kiboro: Kusi Festival imeleta Soko la Usafiri wa Anga Afrika

Aidha, Kiboro ameipongeza Serikali ya Kenya inayoongozwa na Rais William Ruto ambaye amekuwa mstari wa mbele kushiriki kampeni za upandaji miti zinazosaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi.

“NMG imekuwa kipaumbele kwa zaidi ya miaka 35 kwenye kupambana na mabadiliko ya Tabia nchi ambayo yamekuwa yakiathiri mazingira yetu na bara letu kwa ujumla,” amesema.

Kiboro, amewataka Waafrika kutatua changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na sio kusubiri watu wa bara lingine waje wawatatulie.

“Najua Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP-27) umependekeza suluhu nyingi kwenye kukabiliana na changamoto hizi za mabadiliko ya tabia ya nchi lakini hatuwezi kuwasubiria watu wa magharibi waje kutupatia njia za kukabiliana na matatizo haya kabla sisi hatujaanza kupambana nayo,” amesema.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango ameshiriki tamasha hilo lenye kaulimbiu inayosema “Mabadiliko ya Tabianchi: Kuchunguza Majibu na Suluhu za Kiafrika” kwa njia ya video.