Ochuka arejeshwa Kenya, anyongwa-10

Ochuka akiwa mahakamani

Muktasari:

Toleo lililopita tuliona jinsi Serikali ya Daniel Arap Moi ilivyowakamata watu wengi na wengine kuwekwa kizuizini wakihusishwa na tukio la mapinduzi ya Agosti 1, 1982.


Toleo lililopita tuliona jinsi Serikali ya Daniel Arap Moi ilivyowakamata watu wengi na wengine kuwekwa kizuizini wakihusishwa na tukio la mapinduzi ya Agosti 1, 1982.

Hata hivyo, wakati watu wanakamatwa, kiongozi wa mapinduzi hayo na Sajenti Pancras Oteyo Okumu walikuwa mjini Dar es Salaam walikopatiwa hifadhi ya kisiasa.

Lakini mambo hayakutarajiwa kuendelea kuwa shwari kwa wanajeshi hao wawili kutokana na mazingira ya kisiasa yaliyokuwa yakiendelea katika mwaka huo muhimu kwa Serikali za Tanzania na Kenya.

Hilo lilikuwa ni jaribio kubwa la tatu baada ya lile la Jumamosi kuamkia Jumapili, Januari 18—19, 1964 linalojulikana kama “Maasi ya kijeshi ya mwaka 1964.”

Jaribio la pili lilikuwa la mwaka 1969, baada ya wahaini kula njama kati ya Machi 1968 na Oktoba 1969 za kuipindua Serikali ya Mwalimu Nyerere. Uhaini huo wa mwaka 1969, kesi yake ilifikishwa mahakamani na kuanza kusikilizwa Jumatatu ya Juni 8, 1970.

Miaka 15 baadaye kesi nyingine ya aina hiyo ikatinga mahakamani. Katika kesi hii ya uhaini wa mwaka 1982, ambayo kesi yake ilianza kusikilizwa Januari 21, 1985 na kumalizika Desemba ya mwaka huo, ushahidi uliotolewa mahakamani ilionekana kuwa aliyekuwa kiongozi wa mapinduzi hayo aliitwa Mohamed Mussa Tamimu.

Ushahidi uliotolewa Mahakama Kuu mbele ya Jaji Kiongozi, Nassor Mzavas, ulibainisha kuwa aliyeasisi wazo la mapinduzi ni Kapteni Eugene Maganga, mzaliwa wa Itaga mkoani Tabora, wakati akiwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na ambaye wakati huo akiwa na umri wa miaka 26.

Kapteni Maganga alijiunga na JWTZ mwaka 1976 na kupata mafunzo ya awali Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Makutopora na baadaye mafunzo ya juu katika chuo cha maofisa wa jeshi Monduli na mafunzo maalumu ya kijeshi jijini London, Uingereza.

Kwa jumla, waliofikishwa mahakamani kujibu shtaka la uhaini ni Hatty McGhee, Kapteni Christopher Kadego, Luteni Eugene Maganga na Suleiman Kamando, Kapteni Vitalis Mapunda, Kapteni Roderic Roberts, Paschal Chaika, Luteni John Chitunguli, Luteni Mark Mkude, Kapteni Oswald Mbogoro na Kapteni Zacharia Hans Pope.

Wengine ni Luteni Badru Kajaje, Christopher Ngaiza, Luteni Gervas Rweyongeza, Luteni Otmar Haule, George Banyikwa, Zera Banyikwa, Luteni Nimrod Faraji na Livinus Rugaimukamu.

Baadhi ya wanajeshi hao walikuwa wakisaidiana katika mipango yao ya uhaini na mtu aliyeitwa Thomas Pius Mtakubwa Lugangira ambaye alijulikana pia kwa majina ya ‘Father Tom’ au ‘Uncle Tom’.

‘Father Tom’, mfanyabiashara Mtanzania aliyekuwa akifanyia shughuli zake mjini Nairobi, alikuwa tayari kugharamia mapinduzi hayo. Hakuwa na uhusiano mzuri na Mwalimu Nyerere kwa sababu aliwahi kumfukuza nchini akidai ni shushushu kutoka Uganda.

Wakati mipango ikikamilika, Mwalimu Nyerere alikuwa ziarani nje ya nchi na aliporejea alikwenda moja kwa moja kijijini kwake Butiama kupitia Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

‘Uncle Tom’ aliwashauri wampindue akiwa hukohuko nje ya nchi kabla hajarudi Tanzania, lakini walitaka arudi kwanza, wampindue akiwa hapa.

Asilimia kubwa ya maandalizi ilikuwa imekamilika, kilichobakia ilikuwa ni kumsubiri Rais arejee kutoka Butiama, lakini mpango ukavuja kabla hawajautekelezwa. Askari mmoja aliyelewa aliropoka katika bwalo la jeshi Lugalo. Ikadaiwa alitaja baadhi ya maofisa wakuu wa jeshi waliokuwamo kwenye mpango huo na vyeo watakavyopewa baada ya mapinduzi kufanikiwa.

Miongoni mwa majina yaliyonaswa na maofisa usalama, aliyeonekana kuwa hatari zaidi ni Mohamed Tamimu, ambaye alikuwa amepata mafunzo yake ya kijeshi nchini Cuba. Ndiye aliyepangwa kuwa mdunguaji maalumu kumuua Mwalimu Nyerere. Hivyo ilikuwa ni lazima kwanza kumdhibiti Tamimu kabla ya wengine ili kuzima mapinduzi hayo.

Wahaini walipanga kukutana kwa mara ya mwisho Jumatano ya Januari 6, 1983 ili kujiridhisha na mpango wao wa kumuua Rais Nyerere Jumapili ya Januari 9, 1983, siku ambayo alikuwa akirejea Dar es Salaam. Lakini baadhi ya washiriki wa mpango huo hawakufika kwenye kikao hicho cha siri.

Waliamua kumtuma mwenzao mmoja nyumbani kwa Tamimu eneo la Kinondoni Mkwajuni. Alipofika alikuta nyumba yake imevamiwa na kuzingirwa na polisi wenye silaha.

Katika ushahidi uliotolewa mahakamani, mwanausalama aliyetoa ushahidi kwa jina la Mr X alisema walipofika nyumbani kwake walijaribu kumkamata lakini akawatoroka kwa kuruka ukuta wa nyumba aliyokuwa akiishi.

Purukushani za kumkamata zilipamba moto eneo la Kinondoni Mkwajuni wakati wakimkimbiza. Alidandia gari moja ‘pick-up’ lililokuwa na masanduku ya bia na kuanza kuwarushia wanausalama waliokuwa wakimkimbiza chupa za bia. Kwa maneno mengine risasi zilikuwa zikijibiwa na chupa za bia. Baadaye walifanikiwa kumuua baada ya kuzidiwa nguvu kwa kuzingirwa.

Baada ya kupata habari za kuuawa kwa Tamimu, wapanga mikakati wenzake walitoroka. Baada ya kifo cha Tamimu, akina Maganga walijua mipango yao haikuwa siri tena.

Yeye na mwenzake Kadego waliamua kutoroka nchini kwa kupitia Tanga, Mombasa hadi Nairobi. Waliokamatwa jijini Dar es Salaam ni wale ambao hawakufanikiwa kutoroka.

Lugangira na Hatty McGhee, ambao walijiita makomandoo, baada ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu, walitoroka kutoka Gereza la Keko mjini Dar es Salaam na kukimbilia Kenya. Kutoka huko Kenya Lugangira alitoroka tena akaenda Uingereza.


Kubadilishana wahalifu

Kwa kuwa kulikuwa na makubaliano kati ya Tanzania na Kenya ya kubadilishana wahalifu, ndipo maofisa wa Tanzania wakabadilishana na Kenya Private Hezekiah Ochuka, ambaye alitakiwa Kenya kwa uhalifu alioufanya huko Agosti 1, 1982, ndipo McGhee na wenzake nao wakakabidhiwa kwa Serikali ya Tanzania kuunganishwa na wenzao katika kesi ya uhaini.

Ochuka na Sajenti Okumu walitakiwa na Serikali ya Kenya kwa tuhuma mapinduzi hayo.

Koplo Ochuka na mwenzake, Sajenti Okumu, walikimbilia Tanzania baada ya jaribio lao kushindwa na kujisalimisha kwa mamlaka za Tanzania. Baadaye wawili hao walishinda kesi (extradition case) mahakamani iliyoletwa na Serikali ya Kenya kutaka warudishwe nchini kwao.

Novemba 1983 Ochuka na mwenzake walirejeshwa Kenya baada ya hayo makubaliano ya marais wa nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda kwamba wahalifu wasipewe hifadhi ya ukimbizi. Waliwekwa jela wakisubiri kesi yao iliyoanza Julai 1985 katika Mahakama ya Kijeshi Kambo ya Jeshi ya Langatta.

Ochuka na Okumu walikutwa na hatia ya uhaini. Waliuawa kwa kunyongwa Julai 9, 1987, katika Gereza la Kamiti.

Ingawa bado Kenya ina adhabu ya kifo kisheria, waliopatikana na hatia ya njama za mapinduzi ya Agosti 1, 1982 ni Koplo Bramwel Injeni Njereman, Walter Odira Ojode, Charles Oriwa, Sajini Joseph Ogidiand, Pancras Oteyo Okumu na Hezekiah Ochuka Rabala ambao walikuwa wa mwisho kunyongwa.

Kama zilivyokuwa njama za mwaka 1965 na 1971 dhidi ya Serikali ya Mzee Jomo Kenyatta, mapinduzi ya Agosti 1982 yalimpa Moi fursa ya kuwashughulikia wapinzani wake kwa mkono wa chuma. Viongozi wa mapinduzi na wengine wanaoshukiwa kuhusika na njama hiyo walikamatwa haraka.