R Kelly amwaga chozi akihojiwa, miaka 70 jela inamsubiri

Muktasari:

  • Ni katika mahojiano aliyofanya baada ya kuachiwa kwa dhamana wiki mbili zilizopita

Chicago. Mfalme wa R&B, R Kelly amewamwaga machozi katika kipindi cha televisheni alipoulizwa swali kuhusu tuhuma za kuwatumikisha kingono mabinti wadogo.

Mambo yalikuwa shwari katika mahojiano hayo mpaka mtangazaji wa CBS, Gayle King alipomuuliza kuhusu tuhuma zinazomkabili.

Alianza kumjibu taratibu kabla ya kupandisha ‘mzuka’ na kumwaga machozi akisema anasingiziwa kufanya unyama huo.

Kwa sauti ya ukali alimwambia mtangazaji: “Tumia akili, sahau kuhusu habari zinazoandikwa na blogu, magazeti. Hebu tumia akili yako kidogo, unadhani naweza kufanya upuuzi huo hasa ukiangalia nimeshawahi kuingia matatizo kwa kesi kama hizo.”

Amesema ni  asingejaribu kumtumikisha mwanamke kingono achilia mbali wanawake 10 anavyodaiwa kwa kuwa tayari ameshawahi kuingia matatani.

“Nichukie kwa sababu jamii imeamua kunifanya nionekane mnyama, lakini ukitumia akili yako utagundua kuwa wabaya wangu wanajaribu kutumia tuhuma nilizowahi kuzishinda ili waniharibie, nakwambia sijawahi kufanya unyama huo,” alisema huku akububujikwa na machozi.

Mwaka 2008, mahakama moja nchini Marekani ilimwachia huru katika madai ya kumshirikisha binti mdogo kucheza sinema ya ngono.

Jaji aliyetoa hukumu alisema mahakama inamwachia huru kwa kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kuwa mwanamke anayeonekana kwenye video hiyo kuwa ana umri mdogo.

Tangu mwishoni mwa mwaka jana, wanawake zaidi ya watano wamejitokeza wakidai kutumikishwa kingoni na mwanamuziki huyo.

Mwezi uliopita alifunguliwa mashtaka 10 ya kuwanyanyasa kingono mabinti wa kati ya miaka 13 na 17 na iwapo atapatikana na hatia huenda akafungwa miaka 70.