Raila hatarini kubaki mpweke

Raila Odinga

Muktasari:

  • Madai ya usaliti na mikakati ya Rais wa Kenya, William Ruto kusaka umaarufu katika ngome za upinzani, vinatishia kumwacha mpweke kisiasa kinara wa muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga.

Nairobi. Madai ya usaliti na mikakati ya Rais wa Kenya, William Ruto kusaka umaarufu katika ngome za upinzani, vinatishia kumwacha mpweke kisiasa kinara wa muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga.

Huku vyama tanzu vya Azimio vikilalamikia kuminywa na ODM chini ya uongozi wa Odinga, Rais Ruto amekuwa akijaribu kuwavuta baadhi ya vigogo wa muungano huo upande wake.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio, Rais (Mstaafu) Uhuru Kenyatta amekuwa kimya tangu alipostaafu miezi miwili iliyopita – hali inayosababisha wadadisi wa masuala ya kisiasa kuamini kuwa amejitenga na upinzani.

Hatua ya baadhi ya viongozi wa Jubilee kutishia kujiondoa Azimio pia imeibua maswali kuhusu hatima ya muunganano huo unaojumuisha vyama 26.

Alhamisi iliyopita, wabunge wanane wa Jubilee walishutumu washirika wao wa ODM wakiwataja kuwa ‘matapeli na walaghai wa kisiasa’.

Chama hicho kinachoongozwa na Kenyatta, kinashutumu ODM kwa kuchukua nyadhifa nyingi katika Bunge la Kitaifa na Seneti na kudhalilisha vyama vingine vya Azimio.

Wabunge hao ni Adan Keynan (Eldas), Sabina Chege (Maalumu), Abdi Shurie (Balambala), Fatuma Dullo (Seneta wa Isiolo), Abdi Haji (Seneta wa Garissa), Amos Mwago (Starehe) na Sarah Korere (Laikipia Kaskazini) ambao walidai ODM waliwapokonya nafasi moja katika Tume ya Huduma za Bunge (PSC).

Wabunge hao walitishia kujiunga na muungano tawala wa Kenya Kwanza.

Hata hivyo, Msajili wa Vyama vya Kisiasa Ann Nderitu alisema hajapokea barua kutoka kwa Jubilee ya kutaka kujiondoa Azimio.

“Kufikia sasa kuna vyama vinne pekee ambavyo vimewasilisha barua ya kujiondoa Azimio -- Maendeleo Chap Chap, Pamoja African Alliance (PAA), Movement for Democracy and Growth (MDG) na United Democratic Movement (UDM),” alisema Nderitu.

Siku chache kabla ya kustaafu, Kenyatta aliwaonya viongozi wa upinzani kuwa watajuta iwapo hawataungana na kuunda upinzani wa kupambana na Serikali ya Rais Ruto.