Rais mteule Liberia aahidi mabadiliko

Muktasari:

  • Ameyataja mambo atakayoyapa kipaumbele katika mabadiliko hayo ni pamoja na kushughulikia ufisadi na kukosekana kwa huduma za msingi katika taifa hilo.

Dar es Salaam. Rais mteule wa Liberia, Joseph Boakai amesema utawala wake utaangalia kwa karibu mikataba ya uchimbaji madini ili kuhakikisha kuwa inanufaisha nchi.

Kwa mujibu wa shirika la habari VOA, Boakai ambaye amemshinda aliyekuwa mpinzani wake kwenye mbio za urais, George Weah aliyekuwa akigombea muhula wa pili, katika duru ya pili ya urais kwenye uchaguzi uliofanyika Novemba 14, amesema kinachofuata baada ya kuingia ofisini, ni kushughulikia masuala yanayorudisha nyuma nchi.

Katika mambo anayoyapa kipaumbele katika mabadiliko hayo, ni pamoja na kushughulikia masuala ya ufisadi na kukosekana kwa huduma za msingi katika taifa hilo.

Boakai amesema mbali na kushughulikia ufisadi na ukosefu wa huduma za msingi, pia atashughulikia  eneo muhimu ambalo Waliberia hawajanufaika nalo la sekta ya madini.

Liberia ni miongoni mwa nchi zenye  akiba kubwa ya madini  Afrika Magharibi yakiwamo  almasi, dhahabu, madini ya chuma na mbao.

“Nimeona rasilimali zetu zikinyonywa na maisha ya watu yanabaki kuwa mabaya zaidi, nitaangalia kwa karibu sekta hii ya madini,” amesema mteule huyo.

Alipoulizwa kama hii itajumuisha kupitia upya mikataba ya uchimbaji madini, Boakai amesema mapitio yatafuata iwapo itahitajika kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa matokeo ya asilimia 99.5 ya kura zilizohesabiwa mpaka sasa na kutangazwa na Kamisheni ya Uchaguzi ya Liberia, Boakai ameshinda kwa kupata karibu asilimia 51 ya kura, huku Weah akipata asilimia 49.

George Weah, 57, aliongoza kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi huo mwezi Oktoba, kwa kupata asilimia 43.83 ya kura, na Boakai alipata asilimia 43.44.

Boakai, 78, ni mwanasiasa mkongwe ambaye kuanzia mwaka 2006 hadi 2018 alikuwa naibu wa Ellen Johnson Sirleaf, aliyekuwa rais wa kwanza mwanamke barani Afrika kwa kuchachaguliwa kidemokrasia.

Katika uchaguzi wa mwaka 2017, George Weah ambaye ni mchezaji soka mashuhuri wa zamani alishinda kwa zaidi ya asilimia 61 ya kura.

Tayari Weah amempongeza Boakai kwa ushindi huo. Katika hotuba yake kupitia radio ya taifa, Weah amesema, "Chama cha CDC kimepoteza uchaguzi, lakini Liberia imeibuka mshindi. Huu ni wakati wa kutanguliza mbele masilahi ya taifa, badala ya masilahi binafsi.