Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais wa Senegal avunja Bunge, adai linavutana na serikali yake

Rais wa Senegal, Bassirou Faye.

Muktasari:

  • Rais Bassirou Faye mwenye umri wa miaka 44, alishinda uchaguzi wa Machi 2024 na kuwa kiongozi wa kuchaguliwa mwenye umri mdogo zaidi barani Afrika, chini ya wiki mbili baada ya kuachiliwa kutoka gerezani.

Dakar. Rais wa Senegal, Bassirou Faye amevunja bunge la nchi hiyo linaloongozwa na upinzani akifungua njia kwa uchaguzi wa haraka wa wabunge kufanyika ikiwa ni miezi sita baada ya kuchaguliwa kwake.

Ametaja sababu kubwa ya uamuzi huo ni bunge hilo kuvutana na serikali yake, jambo linalokwamisha utendaji wake hasa katika kutekeleza ahadi alizozitoa wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Uchaguzi mpya utafanyika Novemba 17, 2024, Faye alisema katika hotuba yake kwa njia ya televisheni jana Alhamisi Septemba 12, 2024 ambapo aliwataka wapigakura kukipa chama chake mamlaka ili aweze kutekeleza mageuzi ya kimfumo aliyoahidi.

Wachambuzi wanasema kuwa chama cha siasa cha Rais Faye (PASTEF), kina nafasi kubwa ya kupata wingi wa viti kutokana na umaarufu wake na kiwango chake cha ushindi katika uchaguzi wa rais wa Machi 2024.

Jukwaa la upinzani la Benno Bokk Yaakar likiongozwa na Rais wa zamani, Macky Sall limelaani hatua hiyo wakidai kuwa Faye ameitisha kikao cha bunge chini ya sheria za uongo ili kutangaza kuvunjwa kwa bunge hilo, huku akimshutumu kwa kuvunja sheria.

Rais Faye mwenye umri wa miaka 44, alishinda uchaguzi huo Machi 2024 na kuwa kiongozi wa kuchaguliwa mwenye umri mdogo zaidi barani Afrika, chini ya wiki mbili baada ya kuachiliwa kutoka gerezani.

Bunge lina hadi mwisho wa Desemba 2024 kupiga kura kuhusu bajeti ya mwaka ujao, hata hivyo uchaguzi mpya wa wabunge utafanya iwe vigumu kufikia tarehe hiyo ya mwisho.

Uchaguzi wa rais uliofanyika Machi 2024 uliitia majaribuni sifa ya Senegal kama taifa lenye demokrasia imara katika Afrika Magharibi, eneo ambalo limekumbwa na mapinduzi au majaribio ya mapinduzi.

Faye na Sonko waliachiliwa kutoka gerezani wiki mbili kabla ya uchaguzi huo kufuatia msamaha wa kisiasa uliotangazwa na aliyekuwa Rais wakati huo, Macky Sall.

Kukamatwa kwao kulizua maandamano ya miezi kadhaa na wasiwasi kwamba Sall angewania muhula wa tatu madarakani licha ya ukomo wa mihula.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yalisema watu kadhaa waliuawa na wengine 1,000 walifungwa jela.

Zaidi ya asilimia 60 ya raia wa Senegal wana umri wa chini ya miaka 25 na asilimia 90 wanafanya kazi katika ajira zisizo rasmi.

Senegal imekumbwa na ongezeko la mfumuko wa bei katika miaka ya hivi karibuni na kufanya kuwa vigumu kwao kupata mahitaji muhimu.

Nchi hiyo pia ni chanzo cha wahamiaji wanaokwenda Ulaya na maelfu wanaondoka kila mwaka kwenye mashua za uvuvi kwenda kutafuta maisha.