Russia: Putin, Wegner waingia kwenye majibizano

Muktasari:

  • Majibizano yameibuka kati ya Rais wa Russia, Vladimir Putin na jeshi binafsi la Wegner la nchini humo kutokana na Putin kulishutumu jeshi hilo kwa vitendo vya uhaini.

Russia. Rais Vladimir Putin wa Russia ameingia katika mzozo na jeshi binafsi la Wegner akilituhumu kuigawa jamii, huku akiahidi kutoa adhabu kwa wanaofanya vitendo hivyo.

Katika hotuba kwa Taifa kupitia televisheni leo Jumamosi Juni 24, 2023, Rais Putin amesema mustakabali wa Russia uko hatarini, akielezea vitendo vya waasi kama usaliti.

Bila kumtaja kiongozi wa kundi la Wagner, Yevgeny Prigozhin amesema matamanio makubwa ya baadhi ya watu yamesababisha uhaini nchini humo.

Kiongozi huyo amesema baadhi ya wananchi wamedanganywa na kuingizwa katika tukio la uhalifu akililenga jeshi la Wegner.

Kutokana na tuhuma hizo, Wegner waliweka ujumbe wa sauti kwenye ukurasa wao wa mtandao wa kijamii wa Telegram unaoonekana kuwa jibu la moja kwa moja kutoka kwa Yevgeny Prigozhin baada ya hotuba ya awali ya Rais Putin.

Sauti ya kiume inayofanana na ya Prigozhin inasikika ikisema: "Kuhusu uhaini wa nchi, Rais alikosea sana.  Sisi ni wazalendo wa nchi yetu, tumekuwa tukipigana na tunapigana hata sasa, na hakuna mtu atafanya kama anavyotaka Rais, FSB (huduma ya usalama ya Russia) au mtu mwingine yeyote, tukubali makosa yetu.”

Mara kadhaa kiongozi wa Wegner amekuwa akiishutumu Serikali ya Putin kwa kushindwa kuwapatia vifaa bora na vya kutosha katika vita inayoendelea dhidi ya Ukraine.

Pia wamekuwa wakitishia kuondoa vikosi katika vita hiyo inayoendelea.