Ruto apiga marufuku uingizaji wa mahindi, ngano
Muktasari:
Unaweza kusema kuwa sasa ni afueni kwa wakulima wa mahindi na ngano nchini Kenya baada ya Serikali kupiga marufuku kuagiza bidhaa hizo ili kulinda soko la ndani dhidi ya nafaka zisizo na ubora ambazo kwazo bei ya bidhaa huyumba.
Dar Es Salaam. Rais wa Kenya, William Ruto ameagiza usitishwaji wa utoaji wa vibali vipya vya kuagiza mahindi na ngano kutoka nje, akibainisha kuwa utawala wake utabatilisha uamuzi huo iwapo nchi itakabiliwa na uhaba wa chakula.
Mtandao wa Daily Nation umeripoti kuwa Ruto amebainisha kuwa Serikali yake imetenga KSh4 bilioni kwaajili ya kununua mahindi kutoka kwa wakulima msimu huu, huku wengi wao wakianza kuvuna kabla ya mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza kunyesha baadaye mwezi huu.
"Hakuna vibali vitakavyotolewa kwa wenye vinu vya kusaga nafaka ili waweze kuagiza ngano au mahindi nje ya nchi. Tunafanya hivi ili kuwalinda wakulima wetu, dhidi ya kushuka kwa bei sokoni," Dk Ruto amesema wakati akizungumza na wajumbe kutoka Kaunti za Narok na Samburu, katika Ikulu ya Nairobi.
Ujumbe huo uliongozwa na Magavana, Patrick Ole Ntutu (Narok) na Jonathan Leleliit (Samburu), Mbunge wa Narok Magharibi, Gabriel Tongoy na Mbunge wa Narok Kaskazini, Agnes Pareiyo.
Kwa upande mwingine, Rais Ruto ameonya wakulima kuuza mazao yao kwa wafanyabiashara wa kati kwa bei ya kutupa, akibainisha kuwa Serikali imedhamiria kukusanya mazao ya nafaka kwa bei shindani.
Kwa mujibu wa Mkuu wa nchi hiyo, Serikali yake itatoa vifaa vya kukaushia nafaka, lakini pia itaondoa tozo za kukausha, kama njia mojawapo ya kupunguza upotevu wa mazao hasa baada ya mavuno.
“Vifaa vya kukaushia vitawawezesha wakulima ambao hawako tayari kuuza mazao yao kwenye Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao, ili wakaushe na kuhifadhi mazao hayo,” amefafanua.
Taarifa kutoka Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu nchini humo, inaonyesha kuwa nchi hiyo imekuwa ikiagiza nje wastani wa tani 295,092 za mahindi kila mwaka, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Takwimu hizo pia zinabainisha kuwa, mahitaji ya kila mwaka ya mahindi nchini humo ni magunia milioni 52, ambayo ni kwaajili ya matumizi ya binadamu, uzalishaji wa chakula cha mifugo, mbegu na utengenezaji wa bidhaa nyingine.
Kwa mujibu wa Phanice Khatundi ambaye ni Mwanachama Mwandamizi wa Kilimo katika Kaunti ya Trans Nzoia, anaamini mavuno ya mahindi msimu huu katika kaunti hiyo yanatarajiwa kuwa magunia milioni 5.6, kati ha yao matumizi ya ndani ni magunia milioni 2, huku yanayotarajia kwenda sokoni ni magunia milioni 3.6.
"Tunatarajia mavuno mengi msimu huu na hatua zimewekwa ili kupunguza hasara baada ya kuvuna," amesema Khatundi.
Kwa upande wa Kaunti ya Uasin Gishu, wao wanatarajiwa kuvuna takriban magunia milioni 4.5 ya mahindi, ambapo zaidi ya magunia milioni 2.5 yatapelekwa sokoni.
Kawaida, Kenya huzalisha wastani wa tani 365,600 dhidi ya matumizi ya tani 756,000 za mahindi na hivyo kulazimika kuagiza nakisi hiyo kutoka nje.
Kwa upande wa eneo la Bonde la Ufa, kumezalishwa wastani wa magunia milioni 4.5 ya ngano kutoka kwa katika hekta 127,825 zilizopandwa msimu uliopita. Huku Kaunti ya Uasin Gishu, ikishuka katika kilimo cha ngano kutoka hekta 40,000 hadi hekta 18,000; sababu ikitajwa ni wakulima kujikita katika uwekezaji wenye faida kama vile mahindi, kilimo cha bustani na ufugaji wa ng'ombe wa maziwa.
"Kilimo cha ngano kimeshuka kwa kiasi kikubwa katika miaka 10 iliyopita, hali ambayo imesababisha athari mbaya hasa kwenye gharama ya bidhaa za ngano," imesema ripoti ya kilimo ya kila mwaka ya kitengo cha ugatuzi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Kilimo anayemaliza muda wake Kello Harsama, nchi inatarajia kuvuna magunia milioni 44 ya mahindi msimu huu, huku magunia milioni 23 ya ziada yakitoka eneo la North Rift, kutokana na kuwepo kwa mbolea ya bei nafuu kupitia mpango wa ruzuku wa Serikali.
Akitetea uamuzi wa kuagiza mahindi ya manjano nchini humo, Harsama amabainisha kuwa uagizaji huo ulilenga kusaidia kupunguza gharama ya chakula cha mifugo na sio kuwaumiza wakulima wa mahindi wa ndani.
"Rais William Ruto ameagiza tununue mahindi ya manjano kwa sababu wafugaji wanatatizika na gharama ya juu ya chakula kutokana na uhaba wa malisho. Uagizaji huu utapunguza ushindani wa mahindi meupe ambayo hutumiwa kulisha mifugo yetu," alieleza Katibu Mkuu huyo.
Alisema Wizara ya Kilimo pia imeanza mchakato wa kununua vikaushio 100 ili kuwasaidia wakulima kukausha mazao msimu huu huku kukiwa na hofu ya hasara kubwa baada ya kuvuna kutokana na mvua za El Niño.
Pia amebainisha kuwa vifaa vya kukaushia mazao vitasambazwa katika kaunti mbalimbali ndani ya mwezi ujao, ili kupunguza hasara wanayoipata wakulima baada ya mavuno.
“Tumeagiza vikaushio kutoka nje ya nchi na mzigo wa manunuzi ya kwanza utafika nchini ndani ya siku 30 zijazo, tutakubaliana na uongozi wa kata ambapo tutavipeleka hivi vikaushio... Tuna zaidi ya aina vitano ya vikaushio katika maduka toafauti tofauti, na tayari pesa zimetengwa ili kusaidia wakulima,” amesema Harsama.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB), Joseph Kimote amewahakikishia wakulima kuwa wakala huyo wa Serikali yuko tayari kununua mazao yao mara tu Serikali itakapotangaza bei mpya.
“Tupo tayari kununua mazao ya wakulima mara tu tutakapopata maelekezo kutoka serikalini, hatutaandika tena hundi, tutatumia fedha zitakazokuwepo tu,” amesema Kimote na kubainisha kuwa wakala huyo ana uwezo wa kuhifadhi magunia milioni 20.