Serikali ya Ukraine yakabiliwa na ufisadi katikati ya vita

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy.

Muktasari:

  • Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy aliyechaguliwa kwa kishindo mwaka 2019 kwa ahadi za kubadilisha jinsi taifa hilo la zamani la Kisovieti lilivyotawaliwa, amesema serikali yake imekubali kujiuzulu kwa naibu waziri baada ya uchunguzi kuhusu madai kwamba alipokea rushwa.

Dar es Salaam. Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy amesema ufisadi katika nchi hiyo imekua ni tatizo sugu katika kipindi hiki ambacho taifa hilo linakabiliana na uvamizi wa Russia huku akiahidi kutokomeza ufisadi huo.

Ahadi ya Zelensky ilikuja huku kukiwa na madai ya ufisadi wa ngazi ya juu, ikiwa ni pamoja na ripoti inayotiliwa shaka katika manunuzi ya kijeshi licha ya maafisa kuhimiza umoja wa kitaifa kukabiliana na uvamizi huo.

Kwa mujibu wa Reuters, Umoja wa Ulaya (EU) umefanya mageuzi ya kupambana na ufisadi kuwa moja wapo ya mahitaji yake muhimu kwa uanachama wa Ukraine baada ya kuipa Ukraine hadhi ya kuomba kujiunga na mataifa 27 ya Ulaya Juni 2022.

“Wiki hii itakuwa wakati wa uamuzi sahihi,” amesema Zelenskiy na kuongeza: "Uamuzi tayari yametayarishwa. Sitaki kuyaweka hadharani kwa wakati huu, lakini yote yatakuwa ya haki."

Zelenskiy aliyechaguliwa kwa kishindo mwaka 2019 kwa ahadi za kubadilisha jinsi taifa hilo la zamani la Kisovieti lilivyotawaliwa, amesema serikali yake imekubali kujiuzulu kwa naibu waziri baada ya uchunguzi kuhusu madai kwamba alipokea rushwa.

Zelenskiy hakumtambua ofisa huyo, lakini ripoti za habari zimesema kaimu Naibu Waziri wa Maendeleo ya kanda, Vasyl Lozinskiy alizuiliwa kwa madai ya kupokea rushwa.

Mtazamo mpya wa ufisadi ulihusisha pia Waziri wa Ulinzi, Oleksiy Reznikov baada ya gazeti moja kuripoti kwamba wanajeshi walidaiwa kupata chakula kwa bei iliyopanda zaidi.

Wizara ya Reznikov ilitaja madai hayo kuwa ya uongo na kamati ya Bunge imetakiwa kuchunguza.