Sierra Leone yapitisha sheria ya ajira kwa wanawake

Rais wa Sierra Leone, Julius Bio.

Muktasari:

  • Rais wa Sierra Leone, Julius Bio amepitisha sheria inayoyalazimisha mashirika ya umma na yale ya kibinafsi kuweka asilimia thelathini ya ajira kwa wanawake.

Freetown. Katika juhudi za kuleta usawa wa kijinsia nchini Rais wa Sierra Leone, Julius Bio amesaini muswada wa sheria utakaolazimisha mashirika ya umma na sekta binafsi kuwaajiri wanawake kwa asilimia 30.

Wanawake wengi nchini humo wanakabiliwa na ubaguzi wa kimfumo, ambao unawanyima haki ya kuajiriwa.

Kwa mujibu wa Sauti ya Amerika (VOA), Rais Bio amesema kuwa, atashughulikia ipasavyo ukosefu wa usawa wa kijinsia wanawake wapate haki sawa za kupata kazi.

Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch limesema wanawake nchini humo ni kawaida kufutwa kazi endapo watapata ujauzito.

Wanawake nchini humo wanakabiliwa na viwango vya juu vya ukatili wa kingono ikiwemo ubakaji.

Vilevile sheria hiyo mpya inalenga pia kuboresha mfumo wa kutoa mikopo kwa wanawake nchini humo ambao wamekuwa wakikosa kabisa mikopo